Mtoto wa miezi mitatu, Ng’wanza Samweli, amekufa baada ya kukwapuliwa
na fisi kutoka mgongoni mwa mama yake wakiwa njiani kwenda nyumbani
kwao katika kijiji cha Ngugunu, wilayani Meatu mkoa wa Shinyanga.
Fisi huyo aliwashambulia mama na mtoto huyo katika kijiji hicho kilichoko kata ya Kisesa mkoani Shinyanga.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Shinyanga, Gemini Mushy alisema tukio hilo ni la Mei 25 saa
1:30.
“Ilikuwa saa 1:30 usiku wa Mei 25, wakati mama wa Ng’waza alipostuka
kuona mwanawe akitolewa mgongoni na fisi aliyetokomea naye
kusikojulikana,” alisema.
Kamanda alisema polisi pamoja na wanakijiji waliendesha msako na
kufanikiwa kupata baadhi ya viungo vya Ng’wanza, umbali wa meta tatu
kutoka mahali alipokwapuliwa.
“ Fisi hatukuweza kumpata lakini tulifanikiwa kupata mabaki ya viungo
vya mtoto huyo kikiwemo kichwa, kifua na tumbo. Miguu na mikono ilikuwa
imekwisha tafunwa pamoja na mifupa,” alieleza.
Kamanda Mushy alisema kuwa, eneo walipovamiwa watu hao lina fisi wengi, ingawa si kawaida kuwavamia wapitanjia.
0 comments:
Chapisha Maoni