Mahakama
ya Mwanzo Kinondoni, imemhukumu Allen Robert (33) kifungo cha mwaka
mmoja jela kwa kosa la kutoroka akiwa chini ya ulinzi mahakamani.
Mtuhumiwa
huyo anayekabiliwa na kesi ya kujaribu kubaka alitoroka akiwa chini ya
ulinzi wa askari magereza mara baada ya kutoka kusikiliza ushahidi wa
kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Hukumu
hiyo imesomwa na Hakimu Marko Mochiwa baada ya askari magereza mwenye
namba B.4296 Koplo John Chale kutoa maelezo ya jinsi Robert alivyotoroka
na kukimbia.
Hakimu
Mochiwa ametoa hukumu hiyo baada ya kupitia maelezo ya mlalamikaji
ambapo amesema kitendo cha kukimbia akiwa chini ya ulinzi ni kinyume
kwa mujibu wa sheria za Jamhuri.
Katika
utetezi wake mtuhumiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana
kesi nyingine inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Awali
mwendesha mashtaka wa polisi alimsomea hati ya mashtaka mtuhumiwa huyo
na kudai kuwa wakati alipokuwa akitoka nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kinondoni baada ya kutoka kwenye kesi ya kubaka akielekea katika chumba
cha mahabusu ghafla alitoroka na kukimbia.
0 comments:
Chapisha Maoni