Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za
kifo cha Mhe. Samuel John Sitta, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kilichotokea usiku wa jana tarehe 6/11/2016 katika
hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alipokuwa
akitibiwa.
Mhe.
Samuel John Sitta, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi
katika Chama na Serikali. Alikuwa Katibu wa CCM na Mkuu wa Mkoa,
Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha uwekezaji, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge, Waziri na Spika.
Mhe.
Sitta alikuwa ni Kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliyejitambulisha
kwa utendaji wenye kufuata falsafa yake ya “kasi na viwango”. Ametoa
mchango mkubwa katika ujenzi wa Chama na Serikali.
Katibu
Mkuu wa CCM Ndg Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai,
familia ya Mhe. Sitta pamoja na Wananchi wa Jimbo la Urambo kufuatia
kifo cha Kiongozi huyu. Tunaungana nao katika msiba huu ambao pia ni
msiba wetu
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Ameni
Imetolewa na:-
CHRISTOPHER OLE SENDEKA (MNEC)
MSEMAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
07 – 11 – 2016