TANZANIA,
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea ya Kusini zimetiliana
saini makubaliano ya pamoja kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme
gridi ya Kaskazini Magharibi inayoanzia mkoani Mbeya, Nyakanazi hadi
Kigoma, yenye msongo wa kV 400 mbapo Serikali ya Korea imeahidi kutoa
Dola za Marekani milioni 50 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 100.18,
kwa ajili ya kugharamia mradi huo.
Hali
kadhalika, Tanzania na Benki ya Exim ya Korea, zimesaini Mkataba wa
mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za marekani milioni 90.092 sawa na
zaidi ya shilingi Bilioni 194 za Tanzania, kwa ajili ya mradi wa Upanuzi
wa Miundombinu ya mfumo wa maji taka Jijini Dar es salaam.
Kwa
upande wa Tanzania, Makubaliano pamoja na Mkataba vimesainiwa na Mhe.
Dkt. Philip Mpango (MB) Waziri wa Fedha na Mipango kwa niaba ya
Serikali, Oktoba 25, 2016 Jijini Seoul nchini Korea Kusini huku upande
wa AfDB, aliye saini ni Rais wa Benki hiyo Adesina Akinwumi, na kwa
upande wa Benki ya Exim, mkataba huo umesainiwa na Mwenyekiti ambaye pia
ni Rais wa Benki hiyo Lee Duk-Hoon.
Akizungumza
mara baada ya kutia saini makubaliano na mkataba huo, Dkt. Mpango
amesema makubaliano na mkataba vilivyosainiwa vina manufaa makubwa kwa
wananchi wa Tanzania.
“Wananchi
wa Upande ule waanze kufurahia kwamba maendeleo yanakuja na hasa
tunaposema maendeleo ya viwanda ambavyo ni lazima vitumie umeme, na
kwamba mradi huu unatarajia kupelekwa hadi Mbeya” Amesisitiza Dkt.
Mpango.
Dkt.
Mpango, amesema kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa pia kwa kuwa serikali
imedhamiria kuufungua ukanda wa Magharibi mwa Tanzania, kwa upande wa
viwanda vya aina mbalimbali.
Kwa
upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uwekezaji) wa Shirika la Ugavi
wa Umeme nchini Tanzania-TANESCO, Decklan Mhaiki, amesema mradi wa umeme
wa Nyakanazi hadi Kigoma utakuwa na urefu wa kilometa 280 na utakapo
kamilika utaondoa changamoto ya shirika hilo kuzalisha umeme unatumika
katika ukanda huo wa Magharibi hususan Kigoma, kwa kutumia majenereta
ambayo uendeshaji wake ni ghali na umeme wake si wa uhakika.
“Kuleta
laini kama hii, kwanza itapunguza gharama kubwa, na umeme wa ziada
utakao zalishwa tunaweza kuuza nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia
Congo, upande wa pili wa Ziwa Tanganyika, lakini kikubwa ni
kuwahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwa na umeme wa uhakika”
ameongeza Bw. Mhaiki.
Akizungumzia
mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya maji taka Jijini Dar es salaam,
Dkt. Philip Mpango, amebainisha kuwa mradi huo unatarajia kuwa na tija
kwakuwa utatatua changamoto ya majitaka kutuama mitaani hasa wakati wa
mvua na kusababisha magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.
Akifafanua
kuhusu mradi huo, Mchumi ambaye pia ni Afisa anayeshughulika na
utafutaji wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Melckzedek
Mbise, amesema kuwa mradi wa maji wa Ruvu unatarajia kuongeza wingi wa
maji Jijini Dar es salaam, utakaosababisha uzalishaji wa maji taka pia
kuongezeka, hivyo mradi huo wa kuondoa maji taka umekuja wakati
muafaka.
“Mradi huu umekuja wakati muhimu na mkopo una masharti nafuu sana” Amesisitiza Bw. Mbise.
Naye
Afisa Mkuu wa utafutaji rasilimali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango
Zanzibar, Sabra Issa Machano, amesema kuwa kati ya nchi 54 za Kiafrika
zinazohudhuria mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea
na Afrika, Mjini Seoul Korea, ni nchi nne tu zilizopewa mkopo na
ufadhili ambazo ni Kenya, Uganda na Ethiopia, huku Tanzania ikipewa
kiasi kikubwa zaidi cha fedha jambo linaloonesha kuwa Tanzania
inakubalika Kimataifa.