Jonas Kamaleki- MAELEZO
Serikali
ya Israel imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli kwa kurejesha uhusiano unaolenga kuziimarisha nchi
hizi mbili kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked wakati wa Kongamano la Tano la Biashara na Uwekezaji kati ya Israel na Tanzania.
“Tunamshukuru
sana Rais Magufuli kwa kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwetu na
tunataraji kuuzindua rasmi juma lijalo”, alisema Waziri Shaked.
Ameongeza
kuwa kwa zaidi ya miongo minne Tanzania na Israel hazikuwa na mahusiano
ya kiuchumi wala ya kisiasa na kuongeza kuwa sasa nchi yao iko tayari
kuwekeza nchini.
Waziri
huyo ameeleza kuwa ni mara yake ya kwanza kufika Afrika na yuko tayari
kuja na familia yake kwa ajili ya kufanya utalii Zanzibar na kwenye
mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Kwa
upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
amewakaribisha waisraeli kuwekeza nchini kwani Tanzania ni kitovu cha
uwekezaji kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kutokana na amani
iliyopo. Pia ameitaja nchi hii kuwa ni lango la biashara kwa nchi za
kiafrika zinazoizunguka.
“Israel
mnakaribishwa kuwekeza hapa Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji ni
mazuri, tunayo ardhi nzuri kwa kilimo, tunayo maziwa, mito kwa ajili ya
kilimo cha umwagiliaji, hivyo hakuna mtakachokikosa endapo mnataka
kuwekeza kwenye kilimo”, alisema Waziri Mwijage.
Waziri
Mwijage amesema Tanzania iko tayari kwa uwekezaji katika kilimo,
viwanda vya dawa, TEHAMA, utalii, uzalishaji wa sukari na uongezaji
thamani kwenye madini, na hivyo kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga
mkono suala la uwekezaji.
Naye
balozi wa Israeli kwa nchi za Tanzania , Kenya, Uganda, Malawi na
Shelisheli, Mhe. Noah Gal Gendler amesema Serikali ya Rais Magufuli
imeonyesha mabadiliko makubwa ya ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kwa
muda mfupi.
“Kwa
kipindi cha zaidi ya miaka 46 hakuna waziri hata mmoja kutoka Israeli
amewahi kuitembelea Tanzania, lakini ndani ya wiki mbili wamefika
mawaziri wawili toka nchini mwetu”, alisema Gendler.
Ameongeza
kuwa katika kuimarisha sekta ya Afya, Israeli itajenga wodi za wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa,
Dodoma, na kituo huduma kwa watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete.
Kongamno
hili ni la tano kufanyika hapa nchini likiwa na lengo la kuonyesha
fursa za uwekezaji zitakazotekelezwa baina ya wafanyabiashara wa Israeli
na Tanzania. Kongamano hili ni fursa kwa sekta binafsi kuitumia vizuri
ili kuongeza tija katika biashara hususan katika kilimo na uwekezaji
katika ujenzi wa viwanda.
0 comments:
Chapisha Maoni