Dar es Salaam. Mfalme Mohammed VI wa Morocco amewasili nchini akiwa na msafara wa ndege tano zilizobeba vifaa vyake, ikiwamo kitanda na mazulia ya kifalme.
Mfalme Mohammed aliwasili jana saa 11:15 jioni akiwa na ujumbe wake wa watu zaidi ya 150, wakitokea nchini Rwanda.
Kabla ya kuwasili kwa ndege yake, zilitangulia ndege mbili ndogo za Morocco zilizokuwa na ujumbe ulioambatana naye. Awali, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga alinukuliwa akisema msafara wa Mfalme huyo ulitanguliwa na ndege mbili zilizobeba vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi yake kwa kipindi chote atakachokuwapo nchini.
“Nadhani mnajua mapokezi ya kifalme yalivyo, wenzetu wanapenda kuandaa wenyewe kila kitu atakachotumia mfalme wao. Ndege mbili zimewasili zikiwa zimebeba vifaa mbalimbali vikiwamo kitanda na mazulia ya kifalme,” alisema Dk Mahiga kabla ya ujio wa Mfalme Mohammed VI.
Mfalme Mohamed VI alipokewa uwanja wa ndege na vikundi mbalimbali vya burudani na raia wa Morocco wanaoishi nchini. Ulinzi uliimarishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa maofisa usalama wa pande zote mbili kwa kuzunguka pande zote za uwanja huo.