test

Jumamosi, 15 Oktoba 2016

Inasikitisha:Hivi ndivyo Fisi wanavyowatesa wanawake Monduli


BAADHI ya wanawake na watoto wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha, wapo hatarini kupoteza maisha kutokana na kukabiliana na wanyama wakali wakiwamo fisi pindi wanapokwenda kutafuta maji usiku.
Hatari hiyo imejitokeza baada ya mabwawa ya maji zaidi ya sita yenye maji ya matumizi ya nyumbani na mifugo, kuharibiwa na mvua zilizonyesha mwaka jana.

Wakizungumza katika Kijiji cha Lepurko, wilayani hapa hivi karibuni baada ya shughuli ya kuwasimika viongozi wapya wa kimila, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliiomba Serikali iwasaidie kukarabati mabwawa hayo ili kunusuru maisha yao.
Akielezea hatari inayowakabili wanawake na watoto, Mepukori Mepashe, alisema tangu bwawa la maji lililopo kijijini hapo kubomolewa na mafuriko, wamekuwa na kero kubwa ya maji.
“Tatizo hilo limesababisha wanawake na watoto kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10 nyakati za usiku kwa ajili ya kutafuta maji.
“Mara kadhaa wanapokuwa njiani, wanakutana na wanyama wakali wakiwamo fisi jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.
“Kwa mfano, hivi majuzi mama mmoja alijikuta akishambuliwa na fisi, kwa bahati nzuri wanawake walikuwa zaidi ya 10 hivyo waliweza kumwokoa.
“Kwa hiyo tunaiomba Serikali itusaidie kukarabati mabwawa haya ili kuondoa kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwani tunahatarisha maisha yetu,” alisema Mepashe.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Boniface Laizer, alisema kama hatua za haraka hazitachukuliwa, kuna uwezekano wa mifugo kufa kutokana na kukosa malisho na maji.
“Hapa wananchi na viongozi wa kimila, wamelazimika kuchanga shilingi milioni sita kwa ajili ya kujaribu kuanza kukarabati bwawa linalotumika kunywesha mifugo na matumizi ya watu,” alisema Laizer.
Naye Mbunge wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga (Chadema), alisema ameshawasiliana na ofisi ya waziri mkuu ili kukarabati bwawa hilo.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx