test

Jumatano, 14 Septemba 2016

Wakurugenzi wapya waambiwa "Jihadharini na wapiga dili"


WAKURUGENZI watendaji nchini wametahadharishwa kuwa makini na wapiga dili kutokana na kuwa jukumu kubwa la kumsaidia Rais katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na wakachape kazi bila kuogopa mtu.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene wakati wa kuapishwa kwa wakurugenzi 13 wa halmashauri za Wilaya, Mji na Manispaa walioteuliwa na Rais John Magufuli, Jumamosi iliyopita.

Wakurugenzi hao waliapishwa na Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati Dodoma, Cathlex Makawia kwa niaba ya Kamishna wa Maadili Jaji mstaafu Salome Kaganda.
Aliwataka kwenda kuwa makini katika utendaji kazi wao hasa wakati wa kusaini mikataba na malipo mbalimbali ili wasidanganyike. “Msifikiri watu watawapenda kapigeni kazi, kazi yenu ni kusimamia vikao, kupokea ripoti na kufanya maamuzi, watu watatumia kila mbinu ili udanganywe, watu wapige hela kwa asili ya kazi yenu hamtapendwa kama mkiona watu wanakupenda sana basi kuna matatizo,” alisema Makawia.

Alisema ugomvi mkubwa kwenye halmashauri ni mgongano wa maslahi.
“Diwani au Mwenyekiti wa halmashauri anataka tenda anatumia nguvu kubwa kupata hiyo tenda ikishindikana inakuwa tabu moja kwa moja" alisema na kuwataka wakurugenzi kuacha kukaa ofisini na badala yake wakatembelee maeneo mbalimbali ili kukagua miradi na kujionea changamoto zilizopo.
Alisema mamlaka ili ziwe na uwezo wa kutambulika kati ya sifa inayotakiwa ni ukusanyaji wa mapato na kwenye eneo hilo, kuna upungufu mkubwa halmashauri nyingi zinaishia asilimia tano za uwezo wa kujitegemea sasa inatakiwa angalau zifikie asilimia 10. Pia alisema kodi za majengo ambazo sasa zinakusanywa mwisho wa siku zitarudi kwenye halmashauri kwani Serikali Kuu iliona inaweza kukusanya vizuri mapato hayo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema uteuzi wa wakurugenzi hao ni heshima kubwa kwa Rais. Pia aliwataka kwenda kuyafanyia kazi maagizo ya viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
"Mkishatekeleza leteni mrejesho wa namna mlivyotekeleza,” alisema na kuongeza kuwa akiwa Waziri mwenye dhamana, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sekretarieti ya Maadili iko chini yake na amekuwa akipata malalamiko kutokana na utendaji wa wakurugenzi ya kiutendaji, kinidhamu na upendeleo.
Wakurugenzi walioapishwa ni Godwin Kunambi (Manispaa ya Dodoma), Elias Ntiruhungwa (Mji Tarime), Mwantumu Dau (Bukoba), Frank Bahati (Ukerewe), Hudson Kamoga (Mbulu), Mwailwa Pangani (Nsimbo), Godfyey Sanga (Mkalama), Yusuf Semuguruka (Ulanga), Bakari Mohamed (Nachingwea), Juma Mnekwa (Kibondo), Butamo Ndalahwa (Moshi), Waziri Mourice (Karatu) na Fatma Latu (Bagamoyo).

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx