test

Jumanne, 20 Septemba 2016

Japan yaahidi kukarabati shule zote zilizoathiriwa na tetemeko mkoani Kagera


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini, Mheshimiwa Masaharu Yoshinda ambaye amemueleza kwamba Serikali yake ipo tayari kukarabati shule zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

Pia imeomba kupatiwa orodha ya mahitaji ya dharura yakiwemo mahema, mablanketi, dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.
 
Balozi Yoshinda ameyasema hayo leo (Jumatatu, Septemba 19, 2016) wakati alipokutana na Waziri Mkuu ofisini kwake Magogoni Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya maafa yalitokea Kagera.
 
Kwa upande wake Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Japan kwa hatua hiyo na kukiagiza Kitengo cha Maafa kilicho chini ya Ofisi yake kuwasiliana na Ubalozi wa Japan nchini na kuwasilisha orodha ya shule zilizoharibika pamoja na mahitaji ya dharura.
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 2.5 za mchele, magodoro 200, mablanketi 100 na fedha taslimu sh. milioni 10 ili kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko hilo.
 
Msaada huo umetolewa na wadau mbalimbali akiwemo Ofisa Utumishi wa Kampuni ya Chang Qing Inernational Investiment Limited ya nchini, Bi. Anna Jiang aliyetoa magodoro 200 yenye thamani ya sh. milioni sita.
 
Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Benki ya Exim, George Shumbusho aliyetooa sh. milioni 10 pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki kati ya Serikali ya Tanzania na China, Bw. Joseph Kahama aliyetoa mchele tani 2.5 pamoja na mabllanketi 100 vyote vikiwa na thamani y ash. milioni 10.
 
Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
 
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 wametibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.
 
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakiiitaji misaada mbalimbali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida kuhusu namna ambavyo Japan inaweza kusaidia waathika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Mazungumzo yao yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dares salaam Septemba 19, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
2 MTAA WA MAGOGONI, 
S. L. P. 3021, 
11410 DAR ES SALAAM. 
JUMATATU, SEPTEMBA 19, 2016

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx