test

Jumatatu, 19 Septemba 2016

Asiyejipenda atafune fedha za tetemeko


Wakati wadau mbalimbali wakiendelea kubuni na kutekeleza mbinu za kupata fedha, nitoe angalizo kwa yeyote ambaye fedha hizo zitapita kwake kabla ya kuwafikia walengwa.

Ni vyema mtu mwenye tamaa ya fedha asijihusishe kabisa na fedha hizi za maafa. Nasema hivi nikirejea na hali halisi ya watu wachache waliojibatiza ‘wajanja’ ambao huvizia matukio kama haya kujinufaisha kiuchumi.
Wapo watu ambao wamejinufaisha kwa fedha za yatima, wajane na zinazolenga kukabili milipuko ya magonjwa. Unaweza kuniuliza ushahidi juu ya madai haya! Ingawa siwezi kukutajia moja kwa moja, lakini matukio yapo na hata watu wa aina hii wapo kwenye jamii, na watu wanawafahamu kabisa. Watu waliolewa ‘ten percent’.
Yeye kila fedha inayotengwa iwe kwa ajili ya mradi au majanga, anahesabu kuwa ndiyo wakati wa mavuno. Hao ‘wajanja wajanja’ ndiyo leo hii natumia nafasi hii kuwahadharisha wawe macho isije wakaondoka na tetemeko la kutumbuliwa.
Tumeshuhudia Serikali ya Awamu ya Tano ilivyo makini katika suala zima la matumizi ya fedha kwa kuhakikisha kila fungu la fedha linatumika kama lilivyopangwa. Tumeshashuhudia watendaji na viongozi wakitumbuliwa kwa madai ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Sasa iweje, kwa atakayetafuna au kutumia vibaya fedha za majanga? Mamilioni haya ya Shilingi yaliyochangwa na yanayoendelea kuchangwa, yanaweza kutengeneza mabilioni ya Shilingi ambayo lengo lake ni kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi na si waathirika wa umasikini.
Mwenye kutaka kukabili umasikini, atafute njia nyingine halali na si ujanja ujanja. Naendelea kusisitiza wale wote wanaoshika fedha hizi za maafa, asiyejipenda, azitafune aone zitakavyomtetemesha.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx