Mkazi wa Mbezi Africana Dar es Salaam, Amani Elikana (32), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni akituhumiwa kumuua Askari wa Usalama Barabarani, Sajenti Mensali wa Kituo cha Polisi Mabatini – Kijitonyama.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu, Caroline Kiliwa, Wakili wa Serikali, Amani Mghamba alidai mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 22 mwaka huu eneo la Kijitonyama.
“Mtuhumiwa inadaiwa kwamba siku hiyo kwa makusudi ulimuua askari mwenye namba D. 8254 Sajenti Mensali kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano,” alidai Mghamba.
Hakimu Kiliwa alisema mtuhumiwa hapaswi kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo hivyo shtaka hilo liliahirishwa hadi Oktoba 4 mwaka huu litakapotajwa tena.