TAHARUKI imeibuka katika majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga
mkoani Rukwa na kusababisha shughuli za mahakamani hapo, zikiwemo za
kusikilizwa mashauri mbalimbali kusimama kwa muda wa takribani dakika
20.
Mtafaruku huo ulitokea baada ya askari kupiga risasi hewani
mahakamani hapo wakati wakimsaka mahabusu aliyedaiwa kutoroka katika
chumba cha mahabusu mahakamani hapo na kujificha darini.
Mwandishi wetu alishuhudia askari polisi wakiwa na bunduki
mikononi wakihaha kumsaka mahabusu huyo ambaye alidaiwa kutoroka kupitia
upenyo uliopo katika chumba cha mahabusi mahakamani hapo.
Mkasa huo ulianzia saa 5 asubuhi na kudumu kwa dakika 20. Hata hivyo,
mahabusu huyo hakuweza kuonekana licha ya jitihada za baadhi ya polisi
kupanda darini kupitia chumba cha mahakama namba mbili bila ya
mafanikio.
Hekaheka za kumsaka mahabusu huyo zilianza pale baadhi ya watumishi
wa mahakamani hapo na mahakimu kudai kusikia vishindo kwenye dari ambapo
mara moja mahabusu waliokuwa kwenye chumba mahakamani hapo
walihesabiwa.
Katika chumba hicho walitakiwa wawe mahabusu 10 lakini walipohesabiwa
kwa mara ya kwanza ilibainika kuwa alikuwa amekosekana mmoja ndipo
msako mkali ulipoanza huku askari wakihaha kumsaka darini.
Hata hivyo walipohesabiwa mara ya pili ilibainika kuwa hesabu yao
ilikuwa imetimu kwamba walikuwa 10 lakini haikubainika nani miongoni
mwao alikuwa ametoroka. Hata mahabusu wenyewe hawakuwa tayari kumtaja.
Habari za kuaminika kutoka mahakamani hapo zinaeleza kuwa baada ya
watumishi wa mahakama hiyo wakiwemo askari polisi na mahakama kusikia
vishindo vya miguu darini waliamini ilikuwa ni ya mahabusu anayedaiwa
kutoroka katika mazingira ya kutatanisha siku tatu zilizopita.
0 comments:
Chapisha Maoni