Harakati za makada wa CCM wanaowania urais kusaka wadhamini mkoani zinaendelea kukumbwa na vituko baada ya wanamgambo wa chama hicho, maarufu kama Green Guards, kumshushia mkong’oto Dk Mussa Muzamill Kalokola aliyeingilia mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya mgombea mwingine.
Tukio hilo lililotokea juzi, ni mwendelezo wa
matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mchakato huo, yakiwamo
ya wanachama kutaka kuchana fomu za mgombea baada ya kunyimwa ‘posho’ na
kada mwingine kukosa wadhamini na kulazimika kuomba chakula cha mchana
kutoka kwa mkuu wa wilaya.
Katika tukio la Tanga, Dk
Kalokola, ambaye pia anadaiwa kushawishi wanachama wasimdhamini mgombea
mwingine wa urais, Bernard Membe, alidaiwa kuvamia mkutano ulioandaliwa
kwa ajili ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kutaka kulazimisha
apewe kipaza sauti kwa ajili ya kuomba wanachama wamdhamini, kitu
ambacho viongozi wa CCM wa wilaya hawakukubaliana nacho na alipoendelea
kung’ang’ania ndipo Green Guards walipoamriwa wamuondoe eneo hilo.
Picha
za video za tukio hilo ambazo zimesambazwa mitandaoni zinawaonyesha
vijana hao wa Green Guards wakimsomba mzobemzobe mgombea huyo,
kumuangusha kwa kumpiga ngwala na mkoba wake wenye stika ya fomu za
mgombea urais, ukionekana kuzagaa chini.
Alipoulizwa kuhusu mkasa huo, Dk Kalokola alikiri kupigwa katika tukio
hilo lilitokea mchana Jumatano ya Juni 17, 2015 alipofika kwenye ofisi
za CCM za Wilaya ya Tanga Mjini, siku ambayo mgombea huyo anadai
alipangiwa na katibu wa wilaya.
Dk Kalokola alisema
baada ya kukabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa na CCM Julai 15 mwaka huu
mkoni Dodoma, alikwenda mkoani Tanga ili kupata wadhamini.
“Tulielekezwa
kuwa makatibu wa CCM wa mikoa ndiyo watakaotutafutia wadhamini siyo
sisi tutafute hivyo mimi tarehe 16 nilikwenda ofisi za CCM kuripoti kwa
katibu wa Mkoa,” alisema.
Hata hivyo, alisema hakuweza
kuonana na Katibu huyo baada ya kuambiwa kuwa hayupo na amemwachia
majukumu hayo katibu wa CCM wa Wilaya ya Tanga Mjini.
Alisema
siku hiyo alikuta wagombea wawili waliofika ofisi hizo wakitaka kupewa
wadhamini ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe na Balozi Amina Salum Ali.
“Hawakutaka hata kunisikiliza shida yangu. Mimi nikaamua kutoa taarifa makao makuu ya CCM,” alisema.
Hata
hivyo, baadaye saa 12:00 jioni alipigiwa simu na katibu wa CCM wilaya
hiyo ya Tanga, akielezwa kuwa aende siku inayofuata asubuhi yaani
Alhamisi.
“Nilienda pale nikasaini kitabu nikawaeleza
kuwa mimi jana (juzi) nilikuwa na kesi ya kupinga Katiba jijini Dar es
Salaam kwa hiyo ningeomba nipate wadhamini siku hiyo hiyo ili
nisafiri,”alisema Dk Kalokola ambaye amefungua kesi akitaka Mahakama Kuu
itangaze kuufuta mchakato wa kupata Katiba mpya kinyume cha utashi wa
chama hicho tawala ambacho kinajisifu kwa kufanikisha mchakato huo.
Dk
Kalokola, ambaye wakati anachukua fomu pia aliiponda CCM akidai inaiba
sera za wapinzani, alisema siku iliyofuata alikubaliwa na kutakiwa
kurejea saa 6:00 mchana.
“Nilipofika nikakutana na
vijana wa Green Gurd wakiwa mlangoni, wakanipiga ngwala wakiniambia huu
ni mkutano wa Lowasa, nikawaambia kuwa mimi nakwenda kumuona Katibu nina
ahadi naye,” alisema.
“Wakaendelea kunipiga lakini
kinachonisikitisha vijana hawa wamekuwa wakija nyumbani kwangu kuniomba
msaada, hata sare walizovaa niliwanunulia mimi… sasa cha kushangaza
wagombea wako 37 kama kila mgombea mmoja siku moja katika kila mkoa
tutamaliza lini zoezi hili?” alihoji.
Alisema kutokana na kipigo hicho, hajaweza kupata wadhamini kwenye mkoa huo ambao alipanga kuanzia kutafuta wadhamini.
“Kesho
(leo) ndiyo nitaanza tena baada ya kutoka mahakamani juzi (Alhamisi).
Hadi sasa sijapata wadhamini hata kwenye mkoa mmoja,”alisema.
Dk Kalokola alisema tukio hilo mbali ya kulitolea taarifa makao makuu ya CCM, pia ameliripoti kituo cha Polisi cha Chumbageni.
Lakini
katibu mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Tanga, Lupakishyo Kapange alisema
kuwa alilazimika kuwaamuru Green Guard wamuondoe kwa sababu mtangazania
huyo alikuwa aking’ang’ania kupewa kipaza sauti ili azungumze katika
mkutano uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya Lowassa.
“Alikuja
hadi nilipokuwa nikitangaza, akataka kuninyang’anya kipaza sauti,
nilipomuomba afuate taratibu za kuandaliwa mkutano wake kwa sababu huu
ulikuwa wa mtangazania mwingine, hakutaka kunielewa akang’ang’ania
nikaamua kuwaita Green Guards wa CCM hapa Tanga wamuondoe,” alisema
Kapange.
Katibu wa CCM wa wilaya, Lucia Mwilu alisema
Dk Kaloloka, ambaye ni mkazi wa Tanga, alifika ofisini kwa mara ya
kwanza Juni 15 wakati wa mapokezi ya Membe na alikuwa akiwazuia
wanachama waliokuwa wakitaka kumdhamini mgombea huyo.
“Nilimwita
na kumuomba afuate taratibu zilizopo kwenye fomu za wagombea urais,
lakini nikakubaliana naye tukutane Juni 16 mchana ili anipe fomu zake
hatimaye niweze kumuandalia taratibu za kudhaminiwa. Hakufanya hivyo
badala yake akamvamia katibu mwenezi,” alisema Mwilu.
Alifafanua
kuwa tukio la kumondoa Dk Kalokola lilitokea saa 7:50 mchana wakati
wanachama wa CCM wakimsubiri Lowassa nje ya jengo la chama hicho la mkoa
wa Tanga, lakini waziri huyo mkuu wa zamani na timu yake aliwasili
Tanga saa 12:00 jioni.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo,
kamanda wa polisi wa mkoa, Zubery Mwombeji alisema Dk Kalokola alitaka
kutumia jukwaa la Lowassa kuwapata wadhamni, wakati ni kinyume na
taratibu za CCM.
Alisema baada ya hapo alikwenda kituo
cha polisi kuomba aruhusiwe kutumia jukwaa hilo, lakini ofisa upelelezi
alimtaka aende kuonana na viongozi wa CCM Kwa sababu suala hilo haliko
chini ya polisi.
Watu walioshuhudia tukio hilo
wameeleza kusitikishwa kwao na kitendo cha kada huyo
kushambuliwa, lakini wamesema baadhi yao walimsihi Dk Kalokola afuate
taratibu lakini hakutaka kuwasikiliza.
0 comments:
Chapisha Maoni