CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Jimbo la Iringa Mjini, vimeingia katika tambo za kisiasa, kila kimoja
kikijigamba kuibuka na ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba,
mwaka huu.
Pamoja
na majigambo hayo, vyama hivyo vimewashambulia watendaji wa Halmashauri
ya manispaa ya Iringa vikisema mbinu zao za kuwakosesha ushindi
hazitafanikiwa.
Wakati
CCM kupitia Katibu wake wa mkoa, Hassan Mtenga kimesema kuna wakuu wa
Idara zaidi ya watano kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wengine
wanakihujumu chama hicho, Chadema kupitia Mbunge wa Jimbo la Iringa
Mjini Mchungaji Peter Msigwa imemrushia kombora Mkurugenzi wa Manispaa
ya Iringa, Ahamed Sawa kikisema ameletwa mjini Iringa kwa lengo la
kudhibiti ushindi wa Chadema.
“Tunazo
taarifa, taarifa za uhakika kwamba, mkurugenzi huyo mpya ameletwa mjini
Iringa kwa lengo la kudhibiti ushindi wa Chadema; mkurugenzi huyo kwa
kushirikiana na CCM wanazuia baadhi ya wapiga kura kujiandikisha katika
maeneo wanayofanyia shughuli zao,” alisema Mchungaji Msigwa.
Naye Mtenga alisema; “Tunazo
taarifa, taarifa za uhakika kabisa juu ya uwepo wa baadhi ya wakuu wa
idara na watumishi wengine wa halmashauri ya manispaa ya Iringa
kukihujumu chama chetu CCM,” alisema.
Alisema
wanachosahau watumishi hao ambao hata hivyo hakuwataja majina ni kwamba
hawajui mishahara wanayolipwa inatokana na juhudi za serikali ya CCM
lakini ndio hao hao wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa na ufisadi
unaoichafua CCM.
Akizungumza
na wanahabari jana, Mtenga alisema Msigwa yuko bungeni Dodoma ili
akawaage wabunge wenzake maana hatarudi katika bunge hilo baada ya
Uchaguzi Mkuu.
Mtenga
alisema katika uongozi wake wa miaka mitano, Mchungaji Msigwa
ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi zikiwemo zile binafsi 84 alizozitoa
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Mtenga
alisema CCM yenye wanachama zaidi ya 70,000 katika jimbo la Iringa
Mjini inatarajia kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu kwa
kutumia mfumo wake imara wa chama katika ngazi zake zote.
“Tunayajua
makosa tuliyofanya wakati wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa hadi Ukawa
wakapata viti vya mitaa 65 huku chama chetu CCM kikipata 126;
niwahakikishie hatutarudia kosa hilo na tunashukuru uchaguzi huo
uliofanyika mwaka jana,” alisema.
Naye
Mchungaji Msigwa aliita wanahabari kuzungumzia kazi ambayo yeye na
wabunge wengine sita wa chama hicho wanaendelea kuifanya mkoani Iringa.
“Kama
mnaangalia Bunge, tumebakiza wabunge watano tu bungeni kwa ajili ya
kuwasilisha taarifa mbalimbali za upinzani. wengine wote tumetawanyika
mikoani kwa ajili ya kuhamasisha watanzania kujiandikisha katika Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema.
Msigwa
alisema wanahamasisha watanzania wote wenye sifa wajiandikishe katika
daftari hilo ili zoezi la kuomba kura litakapowadia kuwepo na kundi
kubwa litakalotumia demokrasia kuchagua viongozi wanaowataka.
“Tunaingia
katika Uchaguzi huo tukiwa na uhakika wa kuunda halmashauri katika
baraza la madiwani la manispaa ya Iringa lakini kwa upande wa mbunge
tuna hakika ya kupata kura zaidi ya 80,000,” alisema na
Huku
wakiwa na imani ya kushinda ubunge na viti vingi vya udiwani
vitakavyowawezesha kuunda halmashauri, Mchungaji Msigwa alisema pamoja
na kuelekeza nguvu za kutosha katika kata zote, lakini za ziada
zitapelekwa katika Kata ya Mlandege inayoongozwa na Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi na ile ya Ilala inayoongozwa na Naibu
Meya, Gervas Ndaki.
Jimbo
la Iringa lina Kata 18, Chadema inadai kuwa ina uhakika wa kushinda
Kata kati ya 14-10 ambazo zitawawezesha kuunda Halmashauri.
Aidha Mchungaji Msigwa alikanusha kutoa ahadi 84 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010.
0 comments:
Chapisha Maoni