Rais
Dkt. John Magufuli amewataka viongozi wa serikali kuacha kutoza ushuru
kwa wananchi wanaosafirisha bidhaa na mazao ambayo hayajafika uzito wa
tani moja, kwakuwa bunge mwaka 2017 lilipitisha sheria ya kufuta tozo
zaidi ya 87 katika sekta ya kilimo.
Rais
Magufuli alisema hayo jana Mei 05, 2018, katika sherehe za uzinduzi wa
daraja Magufuli lililopo katika mto Kilombero mkoani Morogoro, na kusema
kuwa jukumu la serikali ya awamu ya tano ni kutatua kero za wananchi
hasa wakulima na kama Rais wa nchi anazijua kero hizo kwasababu amekua
kiongozi wa serikali kwa zaidi ya miaka 20.
“Nataka
nitoe wito kwa viongozi, ukimuona mtu amebeba magunia 10 ya mpunga
maana yake hayajafika tani moja, mpishe wala usimuangalie mwache
asafirisha mizigo yake, nataka viongozi wenzangu mnielewe nilizunguka
Tanzania nzima kuomba kura kwa ajili ya kuwatetea wananchi, ninafahamu
kero za wananchi, wewe kama ni mtoza ushuru nenda ukalime ukajitoze
ushuru mwenyewe” alisema Rais Magufuli.
Rais
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa serikali haiwezi kuwa kikwazo cha
maendeleo kwa wananchi na kuongeza kuwa anataka daraja hilo liwanufaishe
wananchi wa Morogoro na kuwasihi wakulima kusafirisha bidhaa chini ya
tani moja kama wanataka kuepuka kutozwa ushuru.
Daraja
la Magufuli lipo katika mto Kilombero, barabara kuu ya Kidatu Ifakara
na lina urefu wa mita 384, limegharimu shilingi bilioni 61.2 kwa fedha
za ndani.
0 comments:
Chapisha Maoni