Mkurugenzi
Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana,
amedai mahakamani kwamba Mei 28, 2012 alishangaa kupokea taarifa ya
usuluhishi kutoka Channel 2 Group Corporation (BV1) ya Uingereza kwa
madai ya kuisababishia hasara.
Mshana
alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi dhidi ya mtangulizi wake
katika nafasi hiyo, Tido Mhando, anayekabiliwa na mashtaka ya matumizi
mabaya ya madaraka ikiwamo kuisababishia serikali hasara ya Sh. Milioni
887.1.
Kigogo
huyo ambaye ni shahidi wa tatu wa Jamhuri, alitoa ushahidi wake mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali Mwandamizi Leonard Swai, shahidi huyo alidai kuwa
kampuni hiyo iliwaahidi kuwapatia kazi ya kuhamisha urushaji wa
matangazo kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali katika televisheni.
Mshana
ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC mwaka 2011 hadi 2016 alidai kuwa
alishangaa na kushtuka kwa sababu walipelekewa madai ya pesa nyingi na
walipewa siku 28 kuwa lazima TBC iwe imejibu madai hayo.
Alidai
kuwa aliwasiliana na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TBC iwapo
analifahamu suala hilo au waliwahi kutoa baraka kwa sababu ndio
wasimamizi wakuu wa shirika.
Hata
hivyo, alidai kuwa mwenyekiti wa bodi alieleza kwamba hakufahamu
mkataba huo ulioingiwa kati ya Tido na Channel 2 Group Corporation
(BV1).
"Mwenyekiti
wa bodi alinielekeza niandike barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo labda analifahamu suala
hilo...Wizara ya Habari, ilimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
kuliangalia hilo suala na kutoa ushauri wa kisheria na maelekezo"alidai
shahidi na kuongeza.
"Katika
kumbukumbu zangu Wizara ilitoa maelekezo kwa bodi ya wakurugenzi ya TBC
iitishe kikao cha kujadili na kutoa mapendekezo kwa sababu ilitaka
kujua zaidi kuhusu mkataba huo...mbali na wizara na AG, Msajili wa
Hazina naye alifahamishwa kwa sababu yeye ndiye amepewa dhamana na mali
za shirika pamoja na Wizara ya Fedha ambayo ni mtoa fedha," alidai
Mshana.
Alidai
kuwa katika taarifa ya usuluhishi aliyoipokea, Channel 2 Group
Corporation alidai kuwa TBC imewasababishia kukosa faida ambayo
wangeipata iwapo wangewekeza katika kuhamisha urushaji wa matangazo ya
televisheni kutoka mfumo wa analojia kwenda digital.
Aidha,
bosi huyo wa zamani wa TBC aliomba mahakama kupokea nyaraka za mkataba
unaodaiwa kuingiwa kati ya Tido na Channel 2 Group Corporation, mikataba
ya nyongeza na barua mbalimbali zinazoonyesha uwepo wa Mawasiliano kati
ya TBC, AG, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo, Wizara ya
Fedha na TCRA juu ya suala hilo na kuomba kuzitoa mahakamani kama
vielelezo kwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo.
Wakili wa utetezi, Ramadhani Maleta hakuwa na pingamizi na Mahakama ikavipokea.
Kesi imeahirishwa hadi Mei 18,mwaka huu mashahidi wa upande wa Jamhuri wataendelea kutoa ushahidi dhidi ya Tido.
Katika
kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme
za Kiarabu (UAE), Tido kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa
kutia saini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya
televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila
kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma
na kuinufaisha BVl.
Katika
shtaka la pili, Tido ilidaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20,
2008 alipotia saini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati
ya TBC na BVl.
Katika
shtaka la tatu, ilidaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai,
Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano
kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa
utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika
shtaka la nne, ilidaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido
alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano kwa
kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati
ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika
shtaka la mwisho, ilidaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008
akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh.887,122,219.19.
0 comments:
Chapisha Maoni