Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imepata kibali cha Ajira kwa sekta ya afya nchini cha kuwaajiri wataalam
wa kada mbalimbali za Afya wapatao 8,000.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya.
Dkt.
Mpoki amesema wamepata kibali hicho kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuongeza kwamba Wizara yake inalo
jukumu la kuwapangia vituo vya kazi waombaji wenye sifa kwa mujibu wa
waraka wa Maendeleo ya Utumishi wa Umma Namba 1 wa mwaka 2009 kuhusu
miundo ya utumishi wa kada za afya chini ya Wizara ya Afya.
Aidha,
alisema kibali hicho chenye aina mbili za mwajiri ikiwepo nafasi 6,180
ambazo zimeenda Hospitali zilizo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) kwenye hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati.
Nafasi
1,820 zimeenda Hospitali zilizo chini ya Wizara ya Afya, Hospitali za
Rufaa za Mikoa, Wizara zingine na Taasisi za Umma pamoja na Hospitali ya
Mlongazila na Benjamini Mkapa.
Alitaja
sifa za waombaji wa nafasi hizo kuwa, awe raia wa Tanzania, umri
usiozidi miaka 45, asiwe mwajiri wa Serikali au mwajiriwa wa Hospitali
za Mashirika ya Dini ambaye mshahara wake unalipwa na Serikali na asiwe
ameshawahi kufanya kazi Serikalini na kuacha kazi.
Hata
hivyo, Dkt. Mpoki amewakumbusha wataalam hasa wale wanaosajiliwa na
mabaraza ya kitaaluma kuambatanisha nakala za usajili au leseni ya
kufanya kazi ya taaluma husika wakati wa maombi hayo.
Katibu
Mkuu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano na kueleza kuwa nafasi hizi
8,000 ni juhudi za Serikali za kupunguza uhaba wa rasilimali watu katika
sekta ya afya.
Imetolewa na :
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Afya
11/5/2018
0 comments:
Chapisha Maoni