Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI
imelipa madeni ya wakandarasi na watoa huduma mbalimbali yanayofikia
zaidi ya shilingi trilioni 1.2 katika mwaka huu wa fedha hatua
iliyochangia kuongeza ukwasi wa fedha katika jamii ikiwa ni hatua ya
Serikali ya kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakua kwa haraka.
Hayo
yamesemwa Jijini Dodoma, na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu Kijaji, wakati akifungua rasmi tawi la benki ya ABC,
lililoanzisha huduma zake za kibenki mkoani humo tangu Januari mwaka
huu.
Alisema
kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuwaongezea uwezo wajasiriamali na
wafanyabiashara waliotoa huduma Serikalini ili waongeze mzunguko wa
fedha katika uchumi.
Ametoa
rai kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa za mikopo
inayotolewa na Benki hiyo ambayo riba yake haizidi asilimia 17 ili
waweze kuendeleza shughuli za uzalishaji mali na huduma za jamii kwa
kuwekeza katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
"Ni
matarajio yangu kuwa sehemu kubwa ya mikopo itakayotolewa na Benki yetu
ya ABC, itaelekezwa kwenye sekta ya kilimo na ujenzi wa viwanda vidogo
vidogo, vya kati, mifugo, uvuvi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo
na misitu" alisema Dkt. Kijaji
Dkt.
Kijaji alisisitiza umuhimu wa uwepo wa sekta imara ya fedha
itakayochochea ujenzi wa viwanda vitakavyo saidia kuongeza thamani ya
bidhaa za kilimo pamoja na kukuza ajira kwa vijana.
Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo ya ABC Bw. Imani John, alieleza kuwa
Benki yake yenye mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 67 imeendelea na
jitihada zake za kupanua huduma zake ili kukidhi mahitaji ya kibenki ya
wananchi.
Alisema
kuwa benki yake imeanzisha huduma zake katika Jiji la Dodoma kufuatia
utafiti uliofanyika hivi karibuni unaoonesha kuwa asilimia 13 pekee ya
wakazi wa mkoa huo wanafikiwa na huduma za kipenki, pamoja na uamuzi wa
benki hiyo wa kuunga mkono hatua ya Serikali ya kuufanya mkoa wa Dodoma
kuwa Makao Makuu ya nchi.
Kwa
upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi,
Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde, ameishukuru Benki ya ABC kwa
kupeleka huduma za kibenki karibu na wananchi wa Jiji la Dodoma na
kuwataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za mikopo ili waweze
kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, pamoja na kuipongeza
Benki ya ABC kwa hatua yake ya kusogeza huduma za kibenki kwa wakazi wa
Jiji la Dodoma, amezitaka taasisi nyingine kuwekeza katika sekta hiyo
pamoja na huduma nyingine kama vile ujenzi wa Hoteli za kisasa kwa kuwa
mkoa huo una fursa nyingi ikiwemo ardhi yenye rutuba.
Benki
ya ABC inafanya huduma zake hapa nchini kwa zaidi ya miaka 20 na
inamilikiwa na wanahisa akiwemo TDFC ambaye ni mbia wa ABC Holding Ltd,
anayemiliki asilimia 14.7, kati ya asilimia hizo 14.7, asilimia 68
zinamilikiwa na ABC Holding ltd, na asilimia 32 zinamilikiwa na Serikali
kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.
0 comments:
Chapisha Maoni