test

Alhamisi, 24 Mei 2018

Babu Tale Apelekwa mahabusu kwa muda usiojulikana


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemwamuru mkurugenzi wa kampuni ya Tiptop Connections Company Limited, Hamis Shaban Taletale maarufu kwa jina la Babu Tale, kukaa mahabusu katika kituo cha Polisi akisubiri amri ya kupelekwa kifungoni.

Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Naibu Msajili, Wilbard Mashauri Februari 16, iliamuru Babu Tale na ndugu yake Idd Shaban Taletale wakamatwe na kupelekwa kifungoni baada ya kushindwa kutekeleza hukumu yake.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Agustine Shangwa Februari 18, 2016, iliwaamuru ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250 milioni, Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kwa makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.

Kutokana na amri hiyo ya kuwakamata, Babu Tale alitiwa mbaroni juzi na jana alipelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya amri ya kumpeleka kifungoni, lakini alilazimika kurudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi kwa kuwa Naibu Msajili aliyetoa amri ya kuwakamata hakuwepo.

Amri hiyo ya kumrejesha rumande ilitolewa na naibu msajili wa mahakama hiyo, Ruth Massam hadi hapo Naibu Msajili Mashauri aliyetoa amri ya kuwafunga atakaporejea kutoka Dodoma alikokwenda kikazi.

Kwa kuwa haijulikani ni lini atarejea, Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Abdul Nassib maarufu kama Diamond Platnum, atalazimika kukaa mahabusu kwa muda usiojulikana mpaka atakaporejea.

Hati ya kuwakamata Babu Tale na ndugu yake ilitolewa April 4, mwaka huu kutokana na maombi ya Sheikh Mbonde kupitia wakili wake Mwesigwa Muhingo.

Sheikh Mbonde aliwasilisha maombi hayo baada ya Babu Tale na nduguye kushindwa kutekeleza hukumu hiyo, yaani kumlipa kiasi hicho walichoamriwa na Mahakama wala kubainisha mali za kampuni yao, au zao binafsi, ili zipigwe mnada kulipia fidia hiyo.

Katika kesi ya msingi, Sheikh Mbonde aliieleza Mahakama kuwa Juni 6, 2013 aliingia makubaliano na kampuni hiyo ili irekodi mawaidha yake na kuziuza kisha wagawane faida, lakini baada ya kurekodi masomo saba, walimwambia kuwa walikuwa wameachana na mpango huo.

Alieleza kuwa baadaye alibaini kuwa mikanda ya video ya mfumo wa DVD zenye mawaidha yake zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali huku zikiwa na majina na namba za simu za wakurugenzi wa kampuni hiyo, ndipo akafungua kesi hiyo.

Baada ya Sheikh Mbonde kuwasilisha maombi ya kuwafunga jela Babu Tale na nduguye, mahakama ilimwelekeza Sheikh Mbonde kuwalipia wafungwa hao watarajiwa pesa za chakula mahakamani na kumtaka pesa kwa ajili ya matumizi mengine kuziwasilisha gerezani.

Kwa mujibu wa Mahakama, gharama za kuwahudumia wafungwa hao wakiwa gerezani ni kama ifuatavyo:

Vifaa ambavyo ni taulo ya kuogea Sh12,000; godoro Sh40,000; mto wa kulalia Sh10,000; chandarua Sh13,000; mashuka manne Sh48,000; kandambili (malapa) Sh3000; mswaki na dawa ya meno Sh2,000 ambazo jumla ni Sh128,000 kwa mtu mmoja na kwa watu wote wawili ni Sh256,000.

Chakula, kifungua kinywa Sh7,000; chakula cha mchana Sh8,000; maji lita tatu 3,000, jumla Sh18,000 kwa mtu mmoja kwa siku na kwa wote wawili ni Sh36,000. Wote kwa mwezi ni Sh1,080,000.

Pia, kuna fedha za tahadhari kiasi cha Sh800,000 kwa kila mfungwa na kwa wote wawili jumla ni Sh1,600,000.

Sheikh Mbonde alisema kuwa tayari ameshawalipia wafungwa hao fedha za chakula ya mwezi mmoja kiasi cha Sh1,080,000 na kusema ataendelea kuwalipia kiasi kama hicho kila mwezi.

Alisema fedha za matumizi mengine kama yalivyoainishwa na mahakama, ziko tayari na kwamba hizo ataziwasilisha kwa uongozi wa gereza baada ya wafungwa hao kufikishwa huko.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni