Waziri
Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, amesema Katiba mpya imewekwa pembeni,
kwani watawala hawataki madaraka yao yadhibitiwe na Katiba.
Sumaye,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Kanda ya Pwani, alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam,
kwenye mahafali ya vijana wa chuo kikuu wa chama hicho (Chaso).
Alisema
Katiba inayopendekezwa ni ya wananchi na ilipitishwa na Bunge, lakini
inaonekana si jambo la kipaumbele na wala haitashughulikiwa tena kwa
sababu itawadhibiti watawala.
“Mchakato
wa Katiba mpya umeigharimu nchi fedha nyingi za walipa kodi na kuitupa
ni “makanikia” nyingine, najua Rais John Magufuli amekwishasema yeye
haambiwi la kufanya, lakini sisi tutaendelea kumkumbusha yale ambayo
tunadhani ni muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
“Si
jambo la kupuuzwa. Kama ni la kupuuzwa basi awakamate wote waliohusika
na uamuzi huo, maana ni ubadhirifu unaofanana na ule wa makanikia,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema chama hicho pamoja na washirika wake wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) wataendelea kudai Katiba mpya hadi itakapopatikana.
Alisema
licha ya watawala kueleza kwamba Tanzania ina mfumo wa vyama vingi,
hata hivyo si kweli, bali ina mfumo ‘bandia’ wa siasa za vyama vingi.
“Tuna
mfumo ‘bandia’ wa siasa ya vyama vingi, mfumo wa chama kimoja
kilichovaa ngozi ya vyama vingi, mfumo wa vyama vingi vya siasa ni
lazima ufuate utawala wa sheria na unaolinda, unaoheshimu na kuitetea
Katiba ya nchi ambayo watawala wameapa nayo wakati wa kukabidhiwa
madaraka.
“Ukiona
katika nchi watawala hawatii sheria wala katiba ya nchi, basi hakuna
utawala wa kweli wa vyama vingi vya siasa, bali kuna utawala wa imla
uliovaa ngozi ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
“Tanzania
leo hakuna uhuru wa watu kutoa na kupokea habari kama Katiba yetu
inavyotaka. Ibara ya 18 ambayo inazungumzia “Haki na Uhuru wa Mawazo,” alisema.
Alisema mfumo au demokrasia ya vyama vingi haurusu ubabe katika utawala na uongozi wa nchi.
“Kama
kiongozi anatawala kwa ubabe na vitisho, lazima tukubali kuwa ama
Katiba tuliyonayo siyo sahihi au mfumo uliopo siyo wa demokrasia ya
vyama vingi kivitendo,” alisisitiza.
0 comments:
Chapisha Maoni