Chama
cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kupeleka haraka asilimia 65 ya
fedha za mauzo ya nje ya korosho ghafi kwa Bodi ya Korosho ili zitumike
kama zilivyokusudiwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi,
Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema
kutokupeleka fedha hizo kutasababisha gharama za uzalishaji kwa wakulima
kuongezeka kutokana na ununuaji wa pembejeo kutegemea kwa asilimia 100
katika fedha hizo.
Alisema
jambo hilo lilitokea mwaka jana kupanda kwa dawa aina ya salfa
(Sulphur) katika maeneo mengi kutoka Sh 16,000 hadi kufika Sh 70,000.
“Kwa
mujibu wa sheria ya korosho namba 18 ya mwaka 2009 kifungu 17(A),
inaitaka Serikali kuingiza fedha hizo Bodi ya Korosho lakini fedha hizo
hazijapelekwa kwa miaka miwili sasa,” alisema Shaibu.
Alisema
hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Korosho iliyotolewa na
kamati ya Bunge ya Maji, Kilimo na Mifugo kwa misimu miwili ya mauzo ya
korosho, bodi haijapokea fedha hizo na hivyo kuleta athari mbalimbali
katika kilimo hicho.
Aliongeza
kuwa taarifa hiyo inadai kuwa Bodi ya Korosho haijapokea Sh bilioni 211
ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 wanadai Sh bilioni 91 na 2017/18
wanadai Sh bilioni 110.
“Kutopeleka
fedha hizi kutaathiri Kituo cha Utafiti cha Naliendele kinachozalisha
mbegu bora za korosho na dawa za kudhibiti magonjwa ambacho kinategemea
fedha hizo kwa asilimia 90 kujiendesha kitashindwa kufanya kazi zake kwa
ufanisi,” alisema Shaibu.
Aliongeza
kuwa athari nyingine ni kuvurugika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa
sababu ya usimamizi wa mfuko huo kutegemea fedha hizo kwa asilimia 100.
“Mafunzo
ya kilimo bora kwa wakulima na maofisa ugani yamesimama kwa sasa
kutokana na kukosekana kwa fedha hizo,” alisema Shaibu.
Alisema wanamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kulitolea ufafanuzi suala hili ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza.
Akizungumzia
kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama hicho, Shaibu, alisema umefikia hatua
ya majimbo na kitaifa utafanyika Agosti 25 hadi 27, mwaka huu jijini
Mbeya.
Alisema
chama hicho kinapinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine
Mahiga, aliyoitoa hivi karibuni bungeni kuwa suala la uanachama wa
Sahara Magharibi lina utata wa kisheria katika Umoja wa Afrika na katika
duru za kimataifa.
“Tunapinga
kauli hii kwa kuwa Tanzania tumekuwa mstari wa mbele kuwasaidia kupata
uhuru wa Sahara Magharibi chini ya chama cha ukombozi cha Polisalio,”
alisema Shaibu.
Akizungumza
hivi karibuni, Waziri Mahiga, alisema Polisalio ni chama cha ukombozi
kilichopewa hadhi ya Serikali na uanachama wa Umoja wa Afrika tangu
1982, lakini suala hilo limeanza kuleta utata kisheria.
0 comments:
Chapisha Maoni