Serikali
imemjibu Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), kuwa mradi wa uzalishaji
umeme wa maji wa Stiggler’s George upo katika Ilani Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Majibu
hayo yametolewa bungeni leo na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani,
ikiwa ni siku moja baada ya Nape kuukosoa mradi huo akisema unatekelezwa
wakati haupo kwenye ilani ya chama hicho na kuachwa ule wa gesi ulio
kwenye ilani hiyo.
Akijibu
hoja hiyo na baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge waliokuwa
wakichangia Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu
inayotarajiwa kupitishwa na Bunge leo, Dk. Kalemani amesema ilani ya CCM
imetaja vyanzo vya umeme vitakavyoendelezwa kuwa ni vya maji, gesi,
upepo na makaa ya mawe.
“Haijataja
mradi mmoja mmoja, imeeleza vyanzo vya umeme vitakavyoendelezwa ili
tupate umeme wa uhakika mpaka tuweze kukaa hapa na kusema mwingine
tuuzie majirani zetu,” amesema Dk. Kalemani.
Amesema
katika kile kinachodhihirisha kuwa miradi ya gesi haijatelekezwa, mpaka
sasa megawati 787 za umeme unaotumika unatokana na nishati ya gesi.
“Na
hii itaendelea kwa sababu mpaka 2020 pale Kinyerezi peke yake tutakuwa
na megawati 1,560 zinazotokana na gesi pekee,” amesema Dk. Kalemani.
Akitoa
hoja yake bungeni jana kuhusiana na mradi huo, Nape alisema anashangaa
Serikali kuweka nguvu nyingi kwenye mradi wa umeme wa Stigler’s George
ambao haupo kwenye ilani ya chama hicho na kuachana na umeme wa gesi
ambao waliunadi wakati wa kampeni.
“Sasa
ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani hakuna kabisa kabisa (kwenye
ilani), maana yake ni kwamba hili jambo pengine limenza kuachwa sasa
tuende kwenye Stiglers lakini aje, hatusaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM?
“Lakini
je hatuwasaliti wana Lindi na Mtwara ambao walitupa kura na kutuamini
kwamba gesi yao na uchumi wao uko salama,” alisema Nape.
0 comments:
Chapisha Maoni