test

Jumanne, 10 Aprili 2018

Msukuma Amwagiwa Sifa kwa Kuwatetea Watumishi Darasa la 7 Bungeni


Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kimefunguka na kumwagia sifa Mbunge wa jimbo la Geita Mjini, Joseph Kasheku maarufu kama Musukuma kwa kulivalia njuga suala la watumishi wa umma waliofukuzwa kazi wenye sifa ya darasa la saba, na mpaka serikali kuamua kuwarudisha kazini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Mohamed Mtima  wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari leo baada ya kupita siku moja tokea serikali ilivyotoa kauli yake kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ya kuagiza watumishi wa umma 1,370 walioajiriwa kabla ya Mei 20, 2004 ambao hawakufaulu mtihani wa kidato cha nne, (darasa la saba) na waliondolewa kazini kwa kigezo cha vyeti vya kidato cha nne, warudishwe kazini mara moja na wapewe stahiki zao zote ikiwemo mishahara yao tangu walipoachishwa kazi.

"Suala hili sisi tumeanza muda mrefu kulihangaikia lakini'last week' tuliwaona wabunge walivyokuwa wamechachamaa Bungeni wakiongozwa na Mbunge wa jimbo la Geita Mjini, Joseph Kasheku Msukuma kwa kuweza kulipigia kelele jambo hili.... tunawashukuru sana, kwa maana hata kama lingekuwa lipo kwenye mchakato la kufanyiwa kazi lakini wao waliliongezea kazi zaidi mpaka serikali ikatangaza kuwarudisha kazini", amesema Mtima.

Pamoja na hayo, Mtima ameendelea kwa kusema "kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), napenda kutoa shukrani kwa serikali ya awamu ya tano kwa kuzingatia mapendekezo tuliyowasilisha serikalini Machi 22, 2018 na hatimaye jana yakafanyiwa kazi. 
"Kwa kweli jambo hili tunashukuru sana kwa maana serikali imekuwa sikivu. Pia tunapenda kutoa shukrani kwa Waziri Mkuu kwa namna alivyoweza kutusaidia kipindi tulivyokuwa tunahangaikia mchakato huu".

Kwa upande mwingine, Mtima amesema wanachama wake wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali kwa kuwa umeweza kurudisha matumaini mapya kwa watumishi hao waliofukuzwa kazi hapo awali.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni