Na Fatma Salum-MAELEZO
Serikali
imekutana na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi wenye nia
ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini kwa lengo la
kujadili namna ya kufanikisha mchakato huo.
Mkutano
huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam uliandaliwa na Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kufuatia agizo la
Rais John Pombe Magufuli la kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili
kupata wawekezaji watakaojenga viwanda hivyo.
Akizungumza
na wafanyabiashara pamoja na wadau waliohudhuria mkutano huo, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy
Mwalimu alisema kuwa Serikali imeharakisha mchakato wa kuanzisha viwanda
vya dawa kutokana na changamoto zilizopo kwenye ununuzi wa dawa nje ya
nchi.
“Serikali
kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inakumbana na changamoto kadhaa katika
uagizaji wa dawa nje ya nchi ikiwemo kuletewa dawa baada ya muda mrefu
tangu kuagiza, kupungua kwa thamani ya fedha zetu kwa kubadilisha na
dola za kimarekani pamoja na kuagiza dawa nyingi kwa mkupuo ambazo
hatimaye huharibika kutokana na kukaa muda mrefu,” alisema Ummy.
Pia
Waziri Ummy alibainisha kuwa ni muhimu kuanzisha viwanda vya dawa hapa
nchini kwani bado watanzania wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali
yakiwemo ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
“Mahitaji
ya dawa nchini ni makubwa na mwaka huu wa fedha Serikali imetenga
shilingi bilioni 269 kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba hivyo ni
muhimu kujenga viwanda ili fedha za Tanzania ziendelee kuzunguka hapa
hapa nchini,” alisema Ummy.
Katika mkutano huo wawekezaji 38 wenye
nia ya kujenga viwanda hivyo walijitokeza na Waziri Ummy
aliwahakikishia kuwa Serikali itanunua dawa za ndani lakini lazima ziwe
na ubora na pia viwanda vishirikiane na Chuo cha Sayansi ya Tiba
Muhimbili (MUHAS) ili kuhakikisha ubora wa dawa hizo.
Kwa
upande wake Waziri wa Viwanda ,Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage
aliipongeza sekta binafsi nchini kwa kushirikiana vizuri na Serikali na
kukubali kuhudhuria mkutano huo ili kufanikisha azma ya ujenzi wa
viwanda vya dawa na vifaa tiba.
“Hili
tunalolifanya leo lipo kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa
Miaka Mitano ila tunaharakisha mchakato huu ili ifikapo mwaka 2025 zaidi
ya asilimia 50 ya dawa tunazotumia ziwe zinazalishwa hapa nchini,”
alisisitiza Mwijage.
Aidha
alisema kuwa lengo la Serikali ni kutengeneza sekta binafsi imara na
kuwataka wadau katika sekta hiyo wajiandae kujenga viwanda vya dawa na
Serikali na Taasisi zake zipo tayari kuwasaidia kufanikisha zoezi hilo.
Mkutano
huo wa Serikali na wawekezaji wenye nia ya kujenga viwanda vya dawa
ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa hapa
nchini na Taasisi za Serikali zinazohusika na sekta ya afya zikiwemo
Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Chuo Kikuu
cha Sayansi ya Tiba (MUHAS), Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC).
0 comments:
Chapisha Maoni