UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, leo
tumefika mwisho wa Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 ulioanza Jumanne ya
tarehe 4 Aprili, 2017. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii,
tena baada ya kuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba kikamilifu na kwa
umahiri mkubwa.
Huu ulikuwa ni Mkutano muhimu sana kwa nchi yetu kutokana na jukumu kubwa la kujadili na kupitisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 ulioanza tangu tarehe 1 Julai, 2017. Bajeti hii ambayo ni nzuri na ya kihistoria ni ya pili tu kati ya takribani Bajeti tano za Serikali ya Awamu ya Tano zitakazoandaliwa hadi kifikia Mwaka wa Fedha 2020/2021.
2. Mheshimiwa Spika, wakati
Bunge lako likiendelea, tarehe 13 Aprili, 2017 tulipokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa za vifo vya askari polisi wetu 8 waliopoteza
maisha wakiwa wanalitumikia Taifa kwa kuuawa na kundi la wahalifu
katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilayani Kibiti mkoani Pwani. Askari hao
waliopoteza maisha ni Inspekta Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC
Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub. Pia,
hivi karibuni mwezi Juni, 2017 Askari wetu wawili wa Kikosi cha Usalama
Barabarani walivamiwa na kupigwa risasi na majambazi katika Kijiji cha
Bungu “B” kilichopo Wilayani Kibiti. Aidha, wananchi wetu wengi
wamepoteza maisha kutokana na uhalifu unaofanywa na majambazi waliopo
katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga.
3. Mheshimiwa Spika, natumia
fursa hii kulaani kitendo hicho cha kihalifu, na kutoa pole kwa
Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kuondokewa na vijana hao shupavu. Aidha,
natoa pole kwa familia za wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa wao.
Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu hayakubaliki na wala
hayavumiliki, kwani Askari ndio walinzi wetu sisi pamoja na mali zetu.
Aidha, tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio kwetu
sote, hivyo, Serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo
wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza kukimbia, lakini hawataweza kujificha daima. Tutawakamata!.
4. Mheshimiwa Spika, asubuhi
ya tarehe 6 Mei, 2017, nchi yetu iliamka na simanzi kubwa kufuatia
ajali iliyogharimu maisha ya watu 36, wakiwemo wanafunzi 33, walimu
wawili na dereva wao, waliokuwa kwenye safari ya kimasomo Wilayani
Karatu. Ajali hiyo imezima ndoto za vijana hao na kuacha vilio kwenye
familia zao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema Peponi roho za
marehemu. Aidha, nawaomba wazazi, walezi, walimu na marafiki wa watoto
hao waendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwa mtihani huo mkubwa
walioupata. Naendelea kutoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika na
ukaguzi wa vyombo vya moto vya usafiri kwa wanafunzi na abiria wafanye
ukaguzi wa kina na wa mara kwa mara ili kuliepusha Taifa na ajali
zinazoweza kuzuilika.
5. Mheshimiwa Spika, nchi
yetu pia ilipata pigo la kuondokewa na watumishi wawili wastaafu
waliolitumikia Taifa hili kwa umahiri na uadilifu mkubwa. Watumishi hao
ni marehemu Paul Sozigwa, aliyekuwa Katibu wa Rais wa Awamu ya Kwanza;
na Marehemu Said Mwambungu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. Namwomba
Mwenyezi Mungu awape pumziko la amani marehemu wote baada ya
kulitumikia Taifa letu kwa utumishi uliotukuka na umahiri mkubwa.
SHUGHULI ZA BUNGE
6. Mheshimiwa Spika, katika
Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limejadili na kupitisha bajeti za Wizara
zote 19 na Bajeti nzima ya Serikali Kuu, kupitisha
Maazimio matano (5) ya kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na
kupitisha Miswada ya Sheria mbalimbali, ambayo ni Muswada wa Sheria ya
Fedha za Matumizi; Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka, 2017; Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017; Muswada wa
Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba
inayohusu Maliasili za Nchi, 2017; na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya
Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili.
7. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 499 ya msingi na mengine 1,834 ya
nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na
Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na maswali ya
papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Vilevile,
katika kipindi hiki Ofisi ya Bunge iliendesha Semina mbalimbali kwa
Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa uelewa
mpana wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.
8. Mheshimiwa Spika, Bunge
lako Tukufu pia lilipata fursa ya kuchagua Wawakilishi wa Tanzania
kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo Wabunge tisa
walichaguliwa. Kati ya Wabunge hao, watano ni wanawake, na wanne ni
wanaume. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge hao wataiwakilisha
vema nchi yetu na kwamba watatimiza kikamilifu wajibu wao kwa mujibu wa
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaelekezwa kufanya kazi kwa karibu na
Wabunge hao ikiwa ni pamoja na kuwapa ushirikiano unaostahili ili waweze
kutekeleza vizuri majukumu yao kwenye Bunge hilo.
9. Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu
Spika, Wenyeviti wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu
yake, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge
na Watendaji na Wataalam wa Serikali pamoja na watumishi wa Ofisi ya
Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa kwenye Mkutano huu tena kwa
ufanisi mkubwa.
10. Ninawapongeza
pia na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa maelezo
mazuri ya ufafanuzi waliyotoa wakati wa kujibu maswali mengi ya msingi
na ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu hoja za Kamati za
Kudumu za Bunge na hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge binafsi
ndani ya Bunge zima. Serikali inathamini sana maoni na ushauri wa
Waheshimiwa Wabunge, na tunaahidi kuendelea kuzingatia maoni na ushauri
wao.
AZIMIO LA BUNGE KUUNGA MKONO JITIHADA ZA MHESHIMIWA RAIS
11. Mheshimiwa Spika, tarehe
14 Juni, 2017 Bunge lako Tukufu lilipitisha Azimio la kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, kwa hatua anazochukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya
Serikali katika Sekta ya Madini. Aidha, tarehe 29 Juni, 2017 Bunge lako
lilikubali kwa kauli moja kuridhia mabadiliko ya ratiba ya Mkutano huu
wa Bunge la Bajeti ili kuongeza siku tano za
kazi kwa lengo la kuwezesha kujadili Miswada mitatu ya mwaka 2017
inayohusu kulinda maliasili na rasilimali za Taifa ikiwemo madini. Hii
inadhihirisha kwamba Bunge hili ni lawananchi na linazingatia maslahi ya nchi.
12. Mheshimwa Spika, napenda
kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi
wake mahiri, juhudi na hatua stahiki anazoendelea kuchukua ili
kuhakikisha kwamba Watanzania na Taifa kwa ujumla wananufaika na
rasilimali za Taifa. Nawasihi wananchi wote na viongozi,tuendelee
kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika jitihada zake hizo za kulinda
maliasili za nchi yetu.
HALI YA ULINZI NA USALAMA:
13. Mheshimiwa Spika, kwa
ujumla hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari. Usalama wa raia na
mali zao unaendelea kulindwa, na mipaka yote ya nchi yetu iko salama.
Aidha, vikosi vya ulinzi na usalama viko imara na madhubuti katika
kulinda mipaka na usalama wa nchi yetu. Hata hivyo, wapo baadhi ya
wenzetu wanaotishia usalama wetu kwa kushiriki kwenye vitendo vya
uhalifu wa kutumia silaha. Mathalan, katika miezi ya hivi karibuni,
kumekuwa na mauaji ya kuvizia katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na
Rufiji.
14. Mheshimiwa Spika, dhamira
ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanzania, wakiwemo
wananchi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanakuwa huru kufanya
shughuli zao za maendeleo bila kuhofia usalama wa maisha yao. Serikali
inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu ili kurejesha
hali ya usalama katika maeneo hayo. Tumeongeza doria na vitendea kazi
kwa askari. Vilevile, tumefanya maamuzi ya kuunda Kanda Maalum ya
Kipolisi katika Mkoa wa Pwani itakayojumuisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti
na Rufiji na tayari Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Maalum
amekwishateuliwa. Hivyo, natoa wito kwa raia wema katika Wilaya hizo,
waendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuwezesha watuhumiwa wote
kukamatwa.
15. Mheshimiwa Spika, sanjari
na mikakati ya kudhibiti uhalifu unaofanywa ndani ya nchi, tunaendelea
pia kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka (cross border crimes). Ili
kutimiza jukumu hilo, tunaendelea kuboresha huduma za uhamiaji na
kudhibiti nyaraka zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. Tumeanzisha mfumo
wa kuhakiki nyaraka, hususan vibali vya kuishi nchini pamoja na Hati za
Kusafiria. Vilevile, tumehuisha utaratibu wa kisheria wa kutoa “migrant
pass” kwa wahamiaji walowezi, ili kuweza kuwatambua kwa urahisi. Kwa
jitihada hizi, tutaweza kudhibiti nyaraka za kughushi na kudhibiti
wahalifu wa kimataifa wanaovuka mipaka.
URATIBU WA MAAFA:
16. Mheshimiwa Spika, katika
msimu wa masika, baadhi ya maeneo ya nchi yetu yalipata mvua za juu ya
wastani na hivyo kusababisha maafa na madhara kwa wananchi ikiwemo vifo,
majeruhi na uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu. Mikoa
iliyoathirika zaidi ni Tanga, Arusha, Kagera, Dar es Salaam na visiwa
vya Unguja na Pemba. Kutokana na mvua hizo, watu 15 walipoteza maisha,
78 walijeruhiwa, nyumba 1,845 na majengo 36 ya taasisi mbalimbali
yaliharibiwa katika viwango tofauti. Vilevile, miundombinu ya barabara
48 katika mikoa 11 iliathiriwa na hivyo kuzorotesha kwa muda usafiri na
usafirishaji katika maeneo husika. Aidha, viwanja vya ndege vya Arusha,
Musoma, Ziwa Manyara, Mafia na Sumbawanga navyo viliathiriwa na mvua
hizo. Natoa pole kwa waathirika wote kutokana na kadhia hiyo.
17. Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na athari za mvua hizo, Serikali iligharamia matibabu ya
majeruhi na mazishi ya waliopoteza maisha. Aidha, Serikali imetoa
misaada ya kibinadamu kama vile chakula, dawa, nguo na kufanya
matengenezo ya dharura kwa miundombinu iliyoharibika. Zoezi la ukarabati
wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua linaendelea katika maeneo
mbalimbali ya nchi.
18. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu menejimenti ya maafa hususan
kuzuia na kuweka mipango thabiti ya wananchi kujiandaa na maafa ili
kupunguza athari za maafa pindi yanapotokea. Aidha, tutaendelea kutoa
taarifa za utabiri wa hali ya hewa mara kwa mara na kwa wakati, ili
kutoa fursa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na wananchi kujiandaa.
Vilevile,
tutakamilisha mifumo ya ufuatiliaji wa maafa kwenye kituo chetu
chaUratibu na Mawasiliano wakati wa Dharura; kuainisha na kutambua
maeneo hatarishi kwa maafa pamoja na kuendelea kuijengea uwezo Idara
yetu ya Uratibu wa Maafa.
19. Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 4 Aprili, 2017 hadi tarehe 20 Juni, 2017 Bunge
lako Tukufu lilipokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara, Taasisi mbalimbali za Umma, Mikoa, Mamlaka za
Serikali za Mitaa pamoja na Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Aidha,
Bunge lilipokea na kujadili Hoja ya Serikali kuhusu Hali ya Uchumi wa
Taifa kwa mwaka 2016, Mpango wa Maendeleo pamoja na makadirio ya Bajeti ya Serikali yaMwaka 2017/2018 ya jumla ya Shilingi Trilioni 31.7.
20. Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa
Wabunge wenzangu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango
(Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu
Kijaji (Mb.) kwahotuba nzuri ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2017/2018. Nawapongeza pia Watendaji wa Wizara ya
Fedha na Mipango kwa umakini mkubwa wa maandalizi ya Bajeti
yenyewe. Aidha,
nawapongeza kwa kutoa maelezo na ufafanuzi wa kina kwa hoja za
Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuhitimisha Hoja hiyo. Kipekee kabisa,
nawapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa hoja za maboresho na
kwa kupitisha Bajeti ya Serikali kwa kura nyingi.
21. Mheshimiwa Spika, kura za Waheshimiwa Wabunge kupitisha
Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ni kielelezo kwamba, Bajeti hii inajibu kiu
ya wananchi ambao ninyi Waheshimiwa Wabunge mnawawakilisha. Kupitia
michango yenu na kwa pongezi zenu kwa Serikali, nimepata faraja kwamba
mnathamini na kuheshimu usikivu wa Serikali kwa maoni ya wananchi.
Serikali hii ni sikivu, makini na inazingatia maslahi ya wananchi
walio wengi na hasa wa kipato cha chini. Hivyo, napenda kulihakikishia
Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali siyo tu itaendelea kusikia, bali
itasikiliza na kuchukua hatua, kama tulivyofanya kwenye Bajeti ya mwaka
2017/2018 kwa kufuta kodi mbalimbali za kero hasa katika kilimo na
mifugo ili kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
22. Mheshimiwa Spika, baada
ya Bunge lako kuidhinisha Bajeti ya Serikali, tutahakikisha tunasimamia
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2017/2018. Tayari
tumeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, ambao
unaainisha hatua za utekelezaji, vigezo vya kupima ufanisi na hatua
zinazotakiwa kuchukuliwa katika kukamilisha miradi husika. Vilevile,
tunaandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za miradi ya maendeleo (National
Project Databank) ili kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi na
changamoto zinazoikabili, kwa lengo la kuikwamua. Sanjari na hatua hizo,
Serikali imetoa maelekezo kwamba, Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini
viimarishwe na kupewa nyenzo stahiki ili vifuatilie miradi ya maendeleo
hatua kwa hatua. Shabaha yetu ni kuhakikisha kuwa miradi inasimamiwa
kikamilifu, inaleta tija na kutekelezwa kwa ubora na viwango
vilivyoainishwa kwenye Mikataba.
23. Mheshimiwa Spika,
ni ukweli usiopingika kwamba, mipango tuliyojiwekea haiwezi kufanikiwa,
endapo tutazembea katika ukusanyaji wa kodi na mapato ya Serikali.
Hivyo, Serikali itaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato; kuimarisha
ukusanyaji wa mapato; kudhibiti biashara ya magendo;kuhimiza
matumizi ya mashine za kielektroniki katika ukusanyaji mapato na
kudhibiti udanganyifu katika ukadiriaji wa ushuru wa forodha. Wito
wangu kwa Waheshimiwa Wabunge ni kuhakikisha kuwa mnashirikiana na
Halmashauri kubuni vyanzo vya mapato na kuhamasisha ulipaji wa kodi bila
shuruti.
24. Mheshimiwa Spika, kulipa
kodi ni uzalendo, tuwahamasishe wananchi wenzetu waone fahari kuwa
sehemu ya mafanikio ya nchi yetu kwa kulipa kodi na kuwafichua wakwepa
kodi. Ahadi yetu ni kuendelea kusimamia kila senti itakayokusanywa, ili itekeleze
jukumu lililokusudiwa. Aidha, tutaendelea kuimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha
kwamba fedha zilizotengwa zinatumika kwa umakini na kuleta tija kwa maendeleo ya nchi yetu. Tulipe kodi kwa maendeleo ya nchi yetu!
SEKTA YA KILIMO
Hali ya chakula nchini
25. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hali ya chakula siyo ya kuridhisha sana,
bado kuna maeneo yenye upungufu wa chakula. Pia, yapo maeneo yaliyopata
mvua nyingi ambayo yamepata chakula cha kutosha. Hii ni kutokana na mazao ya chakula katika maeneo hayo kuanza kukomaa. Aidha,
kutokana na wakulima katika baadhi ya maeneo kuanza kuvuna mazao yao,
mwenendo wa bei za vyakula hususan mahindi imeanza kushuka katika masoko
mbalimbali. Hata hivyo, kutokana
na nchi zinazotuzunguka kuwa na upungufu mkubwa wa chakula, na umuhimu
wa kuwa na usalama na kujitosheleza kwa hifadhi ya chakula, ni vizuri
kila kaya ikahakikisha kwamba inakuwa na akiba ya chakula kwa matumizi
ya baadaye. Aidha, tumepiga marufuku usafirishaji mahindi nje ya nchi
bila kibali, badala yake tunahamasisha uongezaji wa thamani ya mazao
badala ya kusafirisha nafaka ghafi. Hii inatokana na kuwepo na maeneo
ambayo hadi sasa hayana chakula cha kutosha. Nashauri Wafanyabiashara
wasambaze mahindi huko. Aidha, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa ya Mipakani
kutekeleza agizo la Serikali la kuchukua hatua kwa watakaokiuka agizo
hilo.
Mfumo mpya wa Usambazaji wa Mbolea
26. Mheshimiwa Spika, Serikali
inajipanga vyema msimu ujao wa kilimo kwa kusambaza pembejeo na
kuhamasisha matumizi ya mbolea. ili kufanikisha azma hiyo, katika bajeti
ya Mwaka 2017/18 Serikali imeamua kuimarisha utaratibu wa upatikanaji
na usambazaji mbolea kupitia Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer Bulk Procurement System).
27. Mheshimiwa Spika, kupitia mfumo huo, mbolea itaagizwa na waagizaji watakaopitishwa kwenye utaratibu wa zabuni, na
wakulima wataweza kununua mbolea hiyo katika maduka ya pembejeo
vijijini kwa bei dira itakayopangwa na Serikali. Mfumo huo mpya utaanza
kwa kuingiza mbolea ya kupandia aina ya DAP na mbolea ya kukuzia aina ya
UREA ambazo zinatumiwa na wakulima wengi. Mbolea za aina nyingine
zitaendelea kuletwa kwa utaratibu wa zamani. Napenda kurejea maelekezo
yangu kwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwamba isimamie kikamilifu
zoezi hili la usambazaji wa mbolea ili kuhakikisha kuwa mbolea
inawafikia wakulima miezi miwili au mitatu kabla ya msimu wa kilimo
haujaanza.
Maboresho kwenye Sekta ya Mifugo
28. Mheshimiwa Spika, pamoja
na idadi kubwa ya mifugo tuliyonayo nchini, lakini mchango wake kwenye
Pato la Taifa na katika kutuingizia fedha za kigeni siyo
wa kuridhisha. Kutokana na hali hiyo, tarehe 15 Juni 2017 nilikutana na
Maafisa Mifugo wa Wilaya zote nchini kwa lengo la kuweka mikakati ya
pamoja ya kuboresha sekta ya mifugo nchini ili iweze kuleta tija na
kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa. Miongoni mwa mikakati tuliyojiwekea ni pamoja
na kuwawezesha wafugaji kupata maeneo mahsusi ya malisho ya mifugo yao
na kuwapatia mafunzo ya stadi za ufugaji bora. Vilevile, tumetoa
maelekezo kwa Maafisa Mifugo kuwatembelea wafugaji ili kuwahudumia na
kuwapa mafunzo ya ufugaji bora. Aidha, tumezindua Mwongozo wa Ufugaji
Bora nchini, ambao utakuwa ni dira ya kuwaongoza wafugaji kuhusu namna
ya kuboresha sekta ya mifugo nchini. Lengo letu ni kuwa na mifugo
michache lakini yenye tija kubwa. Hata hivyo, tumekemea wafugaji
wasilishe mifugo yao katika mashamba yenye mazao ya chakula, na pia
kuchungia kwenye misitu iliyohifadhiwa. Hatua kali zitachukuliwa dhidi
ya watakaokiuka agizo au katazo hilo.
SEKTA YA ARDHI
Upimaji na Umiliki wa ardhi
29. Mheshimiwa Spika, ardhi
isiyopimwa ina thamani ndogo na ni chanzo cha migogoro isiyo ya lazima.
CCM iliona jambo hili, na kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015,
iliielekeza Serikali kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania
kinapimwa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeweka
Mkakati na Mpango Kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga
matumizi bora ya ardhi katika vijiji 1,500 na wilaya 5 kila mwaka.
Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki za
kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi nchini. Katika Mwaka wa Fedha
2017/2018, Serikali imepunguza tozo ya mbele (premium) kutoka asilimia
7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa wananchi
kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na kumilikishwa ardhi.
Kuimarisha Huduma katika Ofisi za Ardhi za Kanda
30. Mheshimiwa Spika, kazi
ya upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila ya rasilimali watu.
Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa kupeleka
wataalam wa kada mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi
stahiki. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za
ardhi katika kanda badala ya kufuata huduma hizo Makao Makuu ya Wizara.
Nawasihi watumishi watakaohamishiwa katika Ofisi za kanda pamoja na wale
waliopo katika Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze
majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia
sekta ya ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi, bila usumbufu
na bila ya kuomba rushwa ya aina yoyote ile.
SEKTA YA WANYAMAPORI
Hifadhi ya Mapori
31. Mheshimiwa Spika, asilimia
28 ya eneo la nchi yetu limetengwa kwa ajili ya kuhifadhi rasilimali za
Taifa ikiwemo misitu, wanyamapori, na utunzaji mazingira kwa ajili ya
matumizi ya binadamu na viumbe hai wakiwemo wanyamapori ambao
wanachangia kwa kiwango kikubwa katika shughuli za utalii. Changamoto
kubwa iliyopo sasa katika mapori yetu ya hifadhi ni uvamizi wa mifugo,
na kwa bahati mbaya kwenye mikoa ya mipakani, mifugo mingi imekuwa
inatoka nchi jirani.
32. Ili
kuhakikisha kwamba Hifadhi za Taifa na mbuga zetu za wanyamapori
zinalindwa kikamilifu. Mwezi Novemba, 2016 niliagiza Wizara ya Maliasili
na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka alama za mipaka (beacons)
kuainisha maeneo yote ya hifadhi nchini kwa lengo la kuondoa migogoro
iliyopo. Baada ya kuweka alama hizo, Serikali imeanza rasmi zoezi la
kuondoa mifugo yote ndani ya hifadhi. Aidha, nimeelekeza kwamba, uwekaji
wa alama au nguzo hizo uhusishe Halmashauri za Wilaya na Ofisi za Wakuu
wa Wilaya. Ramani zinazoonyesha mapori zitumike. Aidha, mapori yote
yaliyohifadhiwa kisheria yaheshimike.
33. Mheshimiwa Spika, kufuatia
kuwepo kwa migogoro baina ya Wafugaji na Wakulima na migogoro baina ya
wafugaji na wahifadhi wa mapori, nimeelekeza kwamba ifikapo mwisho wa
mwezi Julai 2017 Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wabainishe maeneo
yote ya Ranchi za Taifa za Mifugo ambazo hazitumiki na kuzigawa katika
vitalu (blocks) kwa wafugaji ili mifugo mingi iondolewe vijijini
na ipelekwe kwenye maeneo hayo ili Serikali iweze kutoa huduma za ugani
za kisasa huko kwenye hizo blocks.
34. Natoa
wito kwa wafugaji wote nchini kufuata Sheria za Hifadhi za Taifa, Mbuga
za Wanyamapori, maeneo tengefu pamoja na vyanzo vya maji. Mifugo yote
itakayokutwa ndani ya hifadhi, hatua kali zitachukuliwa na kufikishwa
mahakamani. Aidha, tukumbuke kuwa ardhi haiongezeki lakini wafugaji na
mifugo vinaongezeka, hivyo ni lazima tufuge kisasa na tufuge mifugo
michache yenye tija ambayo tutaweza kuihudumia katika maeneo
yatakayotengwa kwa ajili ya ufugaji.
SEKTA YA AFYA
Ununuzi wa dawa na vifaa tiba
35. Mheshimiwa Spika; kama
ambavyo nimekuwa nikisisitiza kuhusu umuhimu wa afya bora kwa wananchi
wetu, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba kwa kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla yaShilingi bilioni 236 zikiwa ni fedha za ndani kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali imetenga fedha za ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 33 kwa
ajili ya chanjo za watoto na makundi maalum. Nitoe rai kwa
wazazi/walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote zinazotakiwa
ili kuwakinga na magonjwa na kuwajengea msingi mzuri wa maisha yao
ya baadaye. Aidha, kila mwananchi ajengeutamaduni wa kupima afya yake
mapema ili kubaini tatizo lake la kiafya mapema, badala ya kusubiri hadi
ugonjwa ufike hatua mbaya ndipo aende hospitali.
Vifo vitokanavyo na uzazi
36. Mheshimiwa Spika, tatizo
la vifo vitokanavyo na uzazi bado ni changamoto kubwa katika nchi yetu.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na
uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Hali hii
haikubaliki na haivumiliki, kwani wanaopoteza maisha ni Watanzania
wenzetu, ni mama zetu, ni wake zetu, ni dada zetu na ni watoto wetu.
Tumesikia maoni na michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu suala hili
wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, bajeti ya Wizara ya
Afya na Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na
Mipango.
37. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imewasikia na kwa hakika inaguswa sana na vifo vitokanavyo na uzazi. Ndio maana Serikali imeamua kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya kuimarisha huduma za Afya ya Mama na Uzazi. Serikali imeamua kwamba, itanunua, kusambaza na kutoa bila malipo dawa
kwa ajili ya uzazi salama katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Hii
ni pamoja na dawa ya kuzuia kutokwa na damu baada ya kujifungua, dawa kwa ajili ya kifafa cha mimba na dawa kwa ajili ya kuongeza damu. Jumla ya shilingi bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Vilevile,
Serikali imejizatiti kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vya afya na
zahanati vijijini pamoja na kuimarisha vituo vyote vya kutolea tiba
nchini kwa lengo la kuboresha huduma za Afya. Hivyo, napenda kuwahakikishia wanawake wote nchini, kwambahakuna
mwanamke mjamzito atakayepoteza maisha kwa kukosa dawa/sindano ya
kuzuia kuvuja damu au kukosa dawa ya kuzuia kifafa cha mimba.
SEKTA YA ELIMU
Kuinua Ubora wa Elimu na Mafunzo
38. Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yangu ya kufungua
mkutano wa saba wa Bunge lako tukufu, unaoahirishwa leo nilieleza
kwa kirefu umuhimu wa watoto wetu kutoa kipaumbele kwa masomo ya
sayansi. Nilisema, endapo watoto wetu hawatasoma masomo ya sayansi,
watabaki kuwa watazamaji kwenye uchumi wa viwanda. Napenda kuliarifu
Bunge lako tukufu, kwamba, Serikali imeanza kutimiza wajibu katika
kuweka mazingira wezeshi kwa watoto wetu kujifunza masomo ya sayansi kwa
vitendo.
39. Tarehe 6 Juni, 2017 nilizindua zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari 1,696 vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9.Vifaa
hivyo vinaendelea
kusambazwa katika shule za Tanzania Bara ambazo zimekamilisha ujenzi wa
maabara. Hivyo, natoa wito kwa wanafunzi kutumia vifaa hivyo kusoma kwa
bidii masomo ya sayansi, na kuvitunza ili vinufaishe wanafunzi wengi
zaidi. Aidha, Halmashauri zote nchini ambazo hazijakamilisha ujenzi
wa maabara zinaelekezwa kukamilisha zoezi hilo mapema, ili vifaa vingine
vitakapoletwa visambazwe haraka.
Elimu Jumuishi
40. Mheshimiwa Spika, sambamba na
jitihada za kuinua ubora wa elimu nchini, Serikali imeendelea kutafuta
suluhu ya changamoto za kujifunzia zinazowakabili wanafunzi wenye
mahitaji maalum. Hivi karibuni Serikali imenunua vifaa kwa ajili ya
wanafunzi wasioona na wenye baki ya usikivu na kuvisambaza katika shule 213 za msingi na 22 za
sekondari. Aidha, Serikali imenunua vifaa vya upimaji ili kubaini
watoto wenye mahitaji maalum ya ujifunzaji kwa mikoa
yote Tanzania Bara. Rai yangu kwa wazazi wenzangu kote nchini, ni
kutumia fursa hii kuwapeleka shuleni watoto wenye mahitaji maalum badala
ya kuwaficha majumbani. Shabaha ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila
mtoto wa Tanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata fursa hiyo bila
kujali uwezo wake wa kifedha au changamoto za kimwili.
Msimamo wa Serikali kuhusu Ujauzito shuleni
41. Mheshimiwa Spika, moja
kati ya mijadala iliyoibua hisia kali wakati wa mjadala wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia ni pamoja na kuwaachisha masomo wanafunzi
waliopata ujauzito shuleni. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla
ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito.
Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito, ni utekelezaji waWaraka
na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa
wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati,
wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na
baadhi ya wanafunzi kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo,
kucheza kamali, kuvua samaki, kuchimba madini, n.k.
42. Mheshimiwa Spika, msimamo
wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na
masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala sio
utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati. Msimamo
huo wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na
masomo yao badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Lengo hili pia nalo ni la kuwaelimisha wazazi kila mmoja aendelee
kumtunza binti yake na kuwafundishe watoto wao mambo mema na maadili
mema ndani ya familia. Wazazi wajishughulishe kikamilifu katika kuweka
katazo kwa watoto kujihusisha na ngono wakiwa na umri mdogo. Dhamira ya
Serikali ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili ya manufaa
yake na Taifa kwa ujumla. Sote tutakumbuka kaulimbiu ya mke wa Rais wa
awamu ya nne, Mama Salma Rashid Kikwete aliyesema: “Mtoto wa mwenzio ni
mwanao.” Kila mzazi hana budi kujikita kuwalea watoto hawa badala ya
kuwafanyisha vitendo ambavyo havistahili.
43. Mheshimiwa Spika,
kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata
elimu. Hivyo, ni lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki
na masomo yake hayakatizwi kwa kupata ujauzito. Serikali imewekeza
kwenye mtoto wa kike. Kifungu Na. 60 (b) cha Sheria ya Elimu Sura ya
353, kinatoa adhabu ya miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa
ujauzito mwanafunzi. Aidha, sheria inatoa adhabu ya kifungo cha miaka
mitano jela au faini ya Shilingi Milioni 5, au vyote kwa pamoja
kwa anayeshiriki kumuozesha mtoto wa shule. Natoa wito kwa Wakuu wa
Wilaya kusimamia utekelezaji wa sheria za nchi zenye lengo la kumlinda
mtoto wa kike. Aidha, nawashauri Waheshimiwa Wabunge, mshirikiane na
Halmashauri zenu kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito kwa watoto wa
shule. Wahamasisheni wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola, ili
wanaowapa wanafunzi ujauzito au kuwakatisha masomo ili waozeshwe wapate
adhabu stahiki.
SEKTA YA MAJI
44. Mheshimiwa Spika, katika
mjadala wa Bajeti moja ya sekta
ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kwamba inahitaji kupewa
kipaumbele cha pekee ni sekta ya maji. Hakika nakubaliana na mtazamo huo
wa Waheshimiwa Wabunge kwani maji ni uhai na kichocheo cha maendeleo
katikasekta
mbalimbali na nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini. Kwa
kuwa suala la maji lilitolewa ufafanuzi wa kina na Mheshimiwa Waziri wa
Maji na Umwagiliaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naomba
Waheshimiwa Wabunge watuelewe kwamba tumewasikiliza na
tumewasikia. Serikali inayo nia ya dhati kuhakikisha kwamba vijiji zaidi
vinapata huduma ya maji.
UBORESHAJI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA NCHINI
45. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kuwa Mamlaka za
Serikali za Mitaa nchini zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa
mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuendeleza
juhudi za ugatuaji wa madaraka kwenda katika vyombo hivyo pamoja na
kuongeza mgawo wa fedha za ruzuku ya maendeleo inayopelekwa katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
46. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Serikali katika mwaka 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo:-
(i) Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 16.985 kwa
ajili ya kuboresha miundombinu ya majengo ya Ofisi na Makazi ya
Viongozi katika Mikoa yote mipya. Katika mgawo huo, Mkoa wa Njombe
umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; Mkoa wa Katavi umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.080; Mkoa wa Simiyu umetengewa jumla ya Shilingi Bilioni 3.775, Mkoa wa Geita umetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.978 na Mkoa wa Songwe umetengewa jumla shilingi bilioni 3.812.
(ii) Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 61.7 kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri 64, Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 28.7 ni kwa ajili ya kukamilisha majengo ya Ofisi katikaHalmashauri 44 na shilingi bilioni 33 ni kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri mpya 20.
Kwa
sasa Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala mpaka
tukamilishe maeneo tuliyoyaanzisha kwa kuboresha miundombinu.
(iii)
Sambamba na hatua hizo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Wazee na Watoto imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha
huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye thamani ya
shilingi bilioni 2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.
(iv) Vilevile, Serikali imeandaa mpango mahsusi wa kuwajengea uwezo
Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa
na Vitongoji ili waweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi katika
kuwahudumia wananchi. Sehemu ya fedha za maendeleo zitatumika kwa ajili
ya kujenga uwezo wa watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
47. Mheshimiwa Spika, juhudi
za Serikali za kuimarisha utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zina
lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua kero zao katika
ngazi hiyo. Aidha, jitihada hizo zimelenga kuongeza kasi ya maendeleo
Vijijini na kuboresha maisha na ustawi wa wananchi wetu. Kwa msingi huo,
natoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya pamoja na Halmashauri, wahakikishe
kwamba malalamiko yote ya wananchi yanatatuliwa haraka katika ngazi
husika. Si vyema na haikubaliki kwa wananchi kusafiri umbali mrefu
kutafuta suluhu za changamoto zao kwa viongozi wa Kitaifa wakati wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo, na zina Viongozi wanaolipwa
mishahara kwa fedha za walipa kodi. Serikali itaendelea kufuatilia
utekelezaji wa maagizo yanayotolewa kuhusu suala hili.
MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
48. Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea na mapambano dhidi ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na
utumiaji wa dawa za kulevya nchini. Tumeendelea kubaini mtandao wa
waingizaji wa dawa hizo hapa nchini na kuchukua hatua stahiki dhidi ya
wahalifu hao. Ili kuimarisha mapambano hayo na kuyaendesha kisayansi,
Serikali imekamilisha uteuzi wa watendaji mahiri wa Mamlaka ya Kupambana
na Dawa za Kulevya wanaojumuisha makamishna wanne waliobobea kwenye
taaluma zao na wenye uzalendo na uzoefu mkubwa kwenye mapambano haya.
49. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi kifupi tangu mwezi Februari, 2017 Mamlaka hii ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu 327.173); cocaine (kilo 26.977); bhangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za
kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini. Aidha, Mamlaka kwa
kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za
kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bhangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.
50. Mheshimiwa Spika,
dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa
kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga
mkono jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa
taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, naendelea kutoa rai kwa wazazi wenzangu kufuatilia mienendo ya
watoto wetu ili wasijiunge katika makundi mabaya ya kujihusisha na dawa
za kulevya. Itakumbukwa kwamba waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni
vijana wenye umri kati ya miaka 15-35, kundi ambalo ni tegemeo kwa
ustawi wa Taifa letu.
51. Mheshimiwa Spika,
Azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa
za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za
kulevya yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio.
Tuungeni mkono kwenye mapambano haya, ili itokomeze kabisa mtandao huo.
SEKTA YA MICHEZO
52. Mheshimiwa Spika, wakati vikao vya Bunge hili vikiendelea, tmu yetu yavijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ilishiriki
na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Barani Afrika ambapo ilimaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na
timu iliyoshika nafasi ya pili. Hata hivyo, kutokana na kanuni
za mashindano hayo, Serengeti Boys haikuweza kuendelea na mashindano
pamoja na matokeo hayo mazuri.
53. Mheshimiwa Spika, binafsi nilifuatilia mechi zote za Serengeti Boys nikiri kwamba, vijana hao wana
vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao. Kwangu mimi vijana wale
ni washindi bila hata ya kupewa taji lolote. Naombanitumie Bunge lako
tukufu, kuwapongeza kwa dhati kudhihirisha kwamba hakuna
linaloshindikana tukiamua. Msisitizo wangu kwa TFF ni
kuendelea kuwatunza vijana hao, na kusimamia vilabu vya michezo nchini
kuwekeza kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache
ijayo.
54. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa
ya ajira kwa vijana wetu. Wiki iliyopita, mkoani
Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa
Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo
wa kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana
wetu kutumia vipaji vyao. Hivyo, tutaendelea kuratibu
michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo
kama somo. Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau mbili
zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha
michezo. Nawapongeza sana Walimu wetu kwa kusimamia vizuri michezo
shuleni. Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote
nchini, wahakikishe kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo
mbalimbali ili kuwapa fursa wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha
na kuinua vipaji vyao, na walimu wanahimizwa wasimamie michezo
mbalimbali shuleni.
55. Mheshimiwa Spika, naomba
nitumie fursa hii kuwashukuru wadhamini waliodhamini michezo yetu ya
UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka huu wa 2017 ambao ni Coca Cola, LAPF na
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa mchango wao mkubwa.
56. Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za michezo
nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa michezo hapa mjini
Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga
uwanja huo.
Serikali
ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia michezo nchini na haitafumbia
macho usimamizi mbovu, na utawala wa michezo usiojali maslahi ya
Taifa.Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo
nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo. Kwa msingi huo, leo hii naelekeza kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini kulifanyia mapitio na kutathmini upya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili
kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini. Pale
itakapodhirika kwamba usimamizi siyo imara, anayo ruhusa ya kulivunja
Baraza hilo na kuunda Baraza jipya.
HITIMISHO
57. Mheshimiwa Spika, kabla
ya kuhitimisha hotuba yangu, naomba nirejee masuala makubwa
niliyoyasisitiza wakati nafungua Mkutano wa Saba wa Bunge lako tukufu.
Masuala hayo niliyoyasisitiza, ambayo naamini bado yana umuhimu hadi
sasa kwa ustawi wa nchi yetu ni kama ifuatavyo:-
(i) Moja, tuendelee kulinda na kudumisha amani nchini ili wananchi washiriki shughuli za maendeleo bila hofu ya usalama wao.
(ii) Pili, jukumu
la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa kila mwananchi.Ni lazima
kila mwananchi afanye kazi kwa bidii na
maarifa, alipe kodistahiki na afichue wanaokwepa kulipa kodi.
(iii) Tatu, tujenge
utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili
kujilinda na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayoyanaigharimu sana nchi
yetu;
(iv) Nne, tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi chetu na vizazi vijavyo;
(v) Tano,
tuzingatie matumizi ya muda, tuongeze nidhamu na uwajibikajituzingatie
muda na kupiga vita tamaduni zote zinazohamasisha uvivu na uzembe; na
(vi) Mwisho, dawa
za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi
yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii kwa kufichua
mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya.
58. Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba
yangu, kwa kuwatakia safari njema Waheshimiwa Wabunge wanaporejea
majimboni kuwaeleza wananchi mambo mengi yaliyojiri hapa Bungeni hususan
kuhusu manufaa ya Bajeti na miswada tuliyoipitisha. Waelezeni
wananchi matarajio yetu kwao na kuwasihi waendelee kutuunga mkono
kwenye jitihada zetu za kuwawekea mazingira wezeshi ya kujikwamua na
umaskini. Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano baina ya
Waheshimiwa Wabunge na Halmashauri zenu, katika ufuatiliaji wa fedha za
maendeleo tunazoleta kwenye Halmashauri, ili zifanye kazi iliyokusudiwa.
Aidha, naitakia maandalizi mema Timu yetu ya Bunge itakayoshiriki
kwenye mashindano ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
yatakayofanyika mwaka huu mjini Dodoma. Tunayo imani kubwa na Timu yetu,
tuwakilisheni vizuri, kama ilivyo kawaida.
59. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 05 Septemba, 2017 siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
60. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
0 comments:
Chapisha Maoni