Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa
Jamhuri ya Uganda Yoweri Museveni kwa pamoja wamekubaliana kutosaini
mkataba wa mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA).
Makubaliano
hayo yamefanyika jana Ikulu, Jijini Dar es Salaam ambapo Rais Yoweri
Museveni yuko nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia
tarehe 25 – 26 Februari, 2017.
Akiongea
na waandishi wa habari Rais Magufuli amesema kuwa mkataba wa EPA hauna
faida bali ni aina nyingine ya ukoloni ambao unataka kurejeshwa kwa nchi
za Afrika.
“Nimeongea
na Rais Yoweri Museveni amekubali kutosaini mkataba wa EPA, nitawaagiza
wataalamu waliosaidia kutupa maelezo juu ya madhara ya mkataba huo
kwenda pia Uganda kuwapa maelezo ambauo waliyatoa kwa Tanzania,” alifafanua Dkt. Magufuli.
Kwa
upande wake, Rais Yoweri Museveni amesema kuwa ameongea na Rais
Magufuli na wamekubaliana kutosaini mkataba huo na kuongeza kuwa suala
la EPA ni lazima lijadiliwe na nchi zote za Afrika Mashariki ili kuwepo
na msimamo wa pamoja kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha
Rais Museni amempongeza Rais Magufuli kwa kulifufua Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya Sita, hivyo amekaribisha shirika
hilo kutoa huduma za usafiri wa anga nchini Uganda kutokana na nchi hiyo
kuwa na uhitaji wa huduma hiyo.
Vilevile
amempongeza Rais Magufuli kwa ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa
(Standard Gauge Railway) kutoka Dar es Salaa mpaka Mwanza na Isaka mpaka
Rwanda ambapo itapelekea ujenzi wa bandari kavu katika mkoa wa Mwanza
hivyo wafanyabiashara wa Uganda kunufaika na bandari hiyo ambayo itakuwa
karibu zaidi kuliko ilivyo kwa Dar es Salaam.
Wakati
huohuo Mawaziri wa Nje kutoka Tanzania na Uganda Balozi Dkt. Augustine
Mahiga na Oryem Henry Okello wamesaini makubaliano ya uhusiano katika
mambo ya Diplomasia baina ya nchi hizo mbili.