Serikali
imesisitiza kuwa hakuna hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) katika sekta zote na hususani sekta za Afya na Elimu
ambayo haitatekelezwa ili kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inafikiwa ipasavyo.
Ahadi
hiyo imetolewa mjini hapa leo na Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Prof. Joyce Ndalichako,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia walipozungumza na waandishi wa
habari kueleza utekelezaji wa hoja za CAG katika sekta zao.
Waziri Ummy: Tunakagua Deni la Wagonjwa Nje
Akieleza
utekelezaji wa hoja mbalimbali katika sekta ya Afya, Waziri Ummy
ameeleza kuwa Wizara ya Afya, baada ya kupata taarifa ya CAG kuhusu
kuongezeka kwa deni la matibabu ya wagonjwa wanaopata rufaa nje ya nchi,
imeamua kufanya uchunguzi wa kina wa kitabibu na kihasibu kujua usahihi
wa deni hili ili kuchukua hatua madhubuti.
Aidha,
amesisitiza kuwa Wizara imekubaliana na ushauri wa CAG wa kuhakikisha
Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa hapa hapa
nchini nchini ili kupunguza gharama. Waziri Ummy ameeleza hatua
mbalimbali zilizochukulia kutekeleza agizo hilo ikiwemo kuanza kutolewa
hapa nchini huduma za upasuaji wa moyo, upandikizaji wa figo, uwekaji wa
vifaa vya usikivu na matibabu ya magonjwa ya mifupa na mishipa ya
fahamu.
Kwa
upande wa huduma za kibingwa katika maradhi ya saratani, Waziri Ummy
alisema tatizo kubwa lililopo sasa ni huduma za kiwango cha juu cha
kupima ugonjwa huo ambazo hazipatikani sehemu nyingi za Afrika. Hata
hivyo alisema katika mwaka mmoja ujao Tanzania itamaliza tatizo hilo
kwani Serikali imetenga Shilingi bilioni 14.5 mwaka ujao wa fedha
kununua mashine ya kupima saratani (PET-CT-SCAN)
Kuhusu
uingizwaji wa bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1.94 kwa
kutumia vibali vya kughushi, Waziri Ummy amesema wameshachukua hatua za
haraka kupitia Bodi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwabaini wote
waliohusika na tayari baadhi wameshakabidhiwa kwenye vyombo vya dola
huku TFDA ikichukua hatua za kujiunga na mfumo wa TRA ili kutambua
nyaraka zisizo halali.
“Wizara
yangu itahakikisha kuwa maoni yote ya CAG yanaendelea kufanyiwa kazi
kwa haraka zaidi ili kuhakikisha hakuna senti ya wananchi katika sekta
ya afya inatumika kinyume na matarajio,” alisema Waziri Ummy.
Prof. Ndalichako: Tunakichunguza Kitengo cha Manunuzi
Akizungumzia
maeneo kadhaa ya sekta ya elimu, Waziri Ndalichako amekubaliana na hoja
mbalimbali za CAG hasa katika eneo la ucheleweshaji wa ujenzi wa miradi
mbalimbali ya elimu ikiwemo ucheleweshaji wa mradi wa ujenzi wa
shilingi bilioni 4.6 katika Chuo cha Ualimu Ndala.
Prof.
Ndalichako amekiri kuwa kuna tatizo ndani ya Kitengo cha Manunuzi
wizarani kwake. Kufuatia hali hiyo, ameagiza uchunguzi kuhusu ufanisi wa
Kitengo hicho ambao utakamilika mwishoni mwa mwezi huu na amesisitiza
kuwa hatasita kuchukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuchelewesha
miradi muhimu ya maendeleo.
Kwa
upande wa changamoto mbalimbali katika utoaji na ufuatiliaji wa madeni
ya mikopo ya Elimu ya Juu, Prof. Ndalichako ameeleza hatua mbalimbali
ambazo Serikali imezichukua ikiwemo kuteua Mkurugenzi Mkuu mpya wa Bodi
ya Mikopo na kuunda Bodi mpya Agosti mwaka jana; mabadiliko ambayo
yameleta mageuzi katika kupunguza muda wa wanafunzi kupata mikopo na
vile vile kuongezeka makusanyo ya madeni ya mikopo.
“CAG
alionesha kuwa miaka ya nyuma Bodi ilikuwa inakusanya kati ya Shilingi
bilioni 32 na 48 za madeni ya mikopo. Lakini tangu iingie Serikali ya
Awamu ya Tano na mabadiliko yaliyofanyika, ukusanyaji umeongezeka hadi
shilingi bilioni 116 mwaka 2016/17 na mwaka huu wa fedha hadi kufikia
Machi, 2018 kiasi cha Shilingi bilioni 132.20 ambazo ni sawa na asilimia
101 ya lengo la mwaka 2017/18,” alisema na kuongeza:
“Nakiri
pia kwamba huko nyuma kulikuwa na udhaifu katika kuwatambua wadaiwa
sugu. Hivi sasa kazi inafanyika ambapo Bodi ya Mikopo imeongeza idadi ya
kuwatambua wadaiwa sugu kufikia 147,231 mwaka 2017/18 kutoka wadaiwa
sugu 48 tu waliobainishwa awali ambapo kati ya waliobainishwa jumla ya
wadaiwa 42,213 wameshaanza kulipa madeni yao ya mikopo.”
Waziri
Ndalichako ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Wizara yake pia
imewaagiza wataalamu na viongozi wote wa taasisi zilizo chini yake
kuhakikisha kuwa wanapitia neno kwa neno taarifa ya CAG ili kuhakikisha
maeneo yote yenye changamoto yanafanyiwa kazi.
Kesho
katika mfululizo wa mawaziri kueleza utekelezaji wa hoja za CAG itakuwa
ni zamu ya Wizara ya Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Wizara
ya Maji na Umwagiliaji.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.


0 comments:
Chapisha Maoni