Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela na
faini ya Sh800,000 ofisa mtendaji wa Kata ya Mkuyuni jijini hapa, James
Chorangirwe baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka na kumlawiti
mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka 12.
Hukumu
hiyo ilitolewa juzi na hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa mahakama
hiyo, Wilbert Chuma baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa
mashtaka. Upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo
alitenda kosa hilo kati ya Novemba 14 hadi 16, 2016.
Kwa
mara ya kwanza, shauri hilo namba 239/2016 lilifunguliwa mahakamani
Novemba 11, 2016 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana ambapo hakimu
aliyekuwa anasikiliza alijitoa baada ya kuwepo madai ya kupanga njama za
kuharibu kesi.
Baada
ya kuwepo madai hayo, Januari 2018, Rais John Magufuli aliingilia kati
kwa kumuagiza mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kufuatilia kwa
karibu upelelezi, uendeshaji na hatima ya shauri hilo ili haki iweze
kutendeka.
Januari
18, 2017, Mongella alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya
Sekou-Toure alikokuwa akitibiwa mtoto huyo ambapo aliusoma hadharani
mbele ya waandishi wa habari na watumishi wa hospitali hiyo ujumbe mfupi
wa simu alioandikiwa na Rais Magufuli kuhusu suala hilo. Katika ujumbe
huo, Mongella aliwataja baadhi ya watendaji, maofisa wa polisi (majina
yao yanahifadhiwa kwa sasa) ambao walituhumiwa kula njama za kuhujumu
upelelezi na mwenendo wa shauri hilo.


0 comments:
Chapisha Maoni