Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) imeweka mipango ya muda mrefu na muda mfupi
ili kuhakikisha huduma ya upandikizaji figo inakuwa endelevu, na
imedhamiria kupandikiza figo kwa wagonjwa zaidi 200 kwa mwaka.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dare es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha
wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuruhusiwa
wagonjwa wawili ambao wamepandikizwa figo Aprili mwaka huu katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Amesema
katika mpango wa muda mfupi, kila mwezi hospitali hiyo itapandikiza
figo wagonjwa watano, hivyo kwa mwaka itakuwa imefanikiwa kupandikiza
figo wagonjwa 60.
“Mipango
ya muda mrefu ni kuwa na sehemu maalum ya upandikizaji figo na hivi
karibuni MNH itaanza ujenzi wa jengo jipya la ghorofa saba na katika
jengo hilo tutatenga sehemu maalum ya upandikizaji figo , kila siku
mgonjwa mmoja atapandikizwa figo, kwa wiki tutakuwa tumepandikiza figo
wagonjwa watano, kwa mwezi wagonjwa 20 na kwa mwaka tutafanikiwa
kupandikiza figo wagonjwa 240,’’ amesema Aminiel.
Kwa
upande wake Mkuu wa kitengo cha Magonjwa ya Figo Muhimbili , Dkt.
Jacqueline Shoo amesema tukio hilo ni la kihisoria kwani mwaka jana
hospitali ilifanikiwa kupandikiza figo mgonjwa mmoja na Aprili mwaka
huu hospitali hiyo imepandikiza figo wagonjwa wanne kwa mfululizo.
Naye
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, Dkt. Onesmo Kisanga amesema
takribani wagonjwa 800 nchini wanasubiri huduma ya upandikizaji figo na
kati ya hao 50 tayari wameandaliwa.
Kwa
upande wao wagonjwa waliopandikizwa figo na kuruhusiwa leo, Bi. Suzana
John na Bi. Asha Athuman Kisebengo wameishukuru Hospitali ya Taifa
Muhimbii pamoja na waaalam wake kwa kuwapatia matibabu ya ubingwa wa
juu ambayo awali hayakuwepo nchini.
0 comments:
Chapisha Maoni