Jeshi
la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia mfanyabiashara wa samaki
aliyefahamika kwa jina la Nicholas Light (25) kwa tuhuma za kumuua
mpenzi wake kwa kumnyonga hadi kufa wilayani Nyamagana.
Hayo
yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa
Polisi, Ahmed Msangi wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari
hii leo Aprili 30, 2018 na kumtaja mwanamke anayedaiwa kuuliwa na
mfanyabiashara huyo kuwa ni Victoria Swai (26) ambaye alikuwa akifanya
kazi katika kampuni inayohusika na masuala ya anga.
Kamanda
Msangi amesema chanzo cha mauaji hayo inasemekana kuwa ni wivu wa
kimapenzi ambapo inadaiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa
anamsaliti kimapenzi, jambo ambalo lilisababisha kuzua ugomvi kati yao
na kupelekea Nicholas kumnyonga mwanamke huyo kwa kumkaba shingo akiwa
ofisini kwake na baadae kukosa pumzi hadi kufariki dunia.
Aidha,
Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali
ya rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi na pindi uchunguzi
utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu ili waweze kufanya
mazishi.
Kwa
upande mwingine, Kamanda Msangi amewapa pole ndugu na familia kwa msiba
walioupata pamoja na kutoa wito kwa wakazi wa jiji la mkoa wa Mwanza
hususani vijana kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi
wanapokuwa kwenye migogoro.
0 comments:
Chapisha Maoni