Karibu nusu ya wananchi pia hawajisikii huru kuwakosoa mawaziri (47%), Wakuu wa Mikoa (46%) na Wakuu wa Wilaya (43%).
Hata
hivyo, idadi kubwa ya wananchi (87%) wanasema wanapaswa kuwa huru
kuikosoa serikali na Rais kwa kufanya maamuzi mabaya na kutosikiliza
ushauri (80%).
Wanaamini
kupitia ukosoaji wanaweza kuisaidia serikali kutofanya makosa (81%) na
si kuwashushia hadhi watendaji wa umma au kuhatarisha umoja (19%).
Vilevile
wananchi hawaungi mkono matumizi ya lugha ya matusi ambapo asilimia 71
ya watanzania hawataki wananchi waruhusiwe kuwaita wafuasi wa chama
chochote cha siasa “wapumbavu au malofa”.
Matokeo
haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wake uitwao Siyo kwa kiasi
hicho? Maoni ya wananchi kuhusu taarifa na mijadala. Takwimu za
muhtasari huu zinatokana na utafiti wa Sauti za Wananchi ambao
huratibiwa na taasisi ya Twaweza.
Sauti
za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za
mikononi. Una uwakilishi wa Tanzania Bara pekee, Zanzibar haihusiki
kwenye utafiti huu. Kwa maelezo zaidi kuhusu mbinu za utafiti huu
tembelea www.twaweza.org/sauti.
Takwimu
za muhtasari huu zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,519 kutoka awamu ya
25 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, na zilikusanywa kati ya
Novemba 7 na Novemba 27 mwaka 2017.
Wananchi
wengi wana imani kubwa na taarifa zinazotolewa na Rais (70%) na Waziri
Mkuu (64%). Idadi ndogo zaidi wanamwamini mwenyekiti wao wa kijiji
(30%), wabunge (wa chama tawala 26%, wa upinzani 12%), na viongozi wa
serikali kwa ujumla (22%).
Wananchi
pia wanaendelea kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa
taarifa: wananchi 7 kati ya 10 wanasema taarifa zinazomilikiwa na
mamlaka za umma ni mali ya umma (70%, juu zaidi kutoka 60% mwaka 2015);
na wananchi 9 kati ya 10 wanasema wananchi wa kawaida wapate taarifa
zinazomilikiwa na mamlaka za umma (86%, juu zaidi kutoka 77% mwaka 2015)
na kwamba kwa kuwapa wananchi uwezo wa kupata taarifa kunaweza
kupunguza rushwa (86%, juu zaidi kutoka 80% mwaka 2015).
Pamoja
na kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa, wananchi 9
kati ya 10 hawajawahi kuomba taarifa kutoka katika ofisi za serikali
(95%), mamlaka za maji (93%), au vituo vya afya (93%).
Wananchi
wameendelea kutumia vyanzo vile vile vya habari bila kuwa na mabadiliko
makubwa isipokuwa kwa upande wa runinga: mwaka 2013 runinga ilikuwa ni
chanzo kikuu cha taarifa kwa 7% ya wananchi, mwaka 2017 ni asilimia 23
ya wananchi.
Hata
hivyo, imani kwa aina mbalimbali za vyanzo vya habari inashuka – radio
kutoka 80% mwaka 2016 hadi 64% mwaka 2017, runinga kutoka 73% mwaka 2016
hadi 69% mwaka 2017 na maneno ya kuambiwa kutoka 27% mwaka 2016 hadi
13% mwaka 2017.
Pamoja
na kushuka kwa imani na vyombo vya habari, wananchi bado wanaunga mkono
uhuru wa vyombo vya habari: wananchi wanasema gazeti lililochapisha
taarifa za uongo ama zisizo sahihi liombe radhi na kuchapisha
marekebisho (62%) badala ya gazeti hilo kufungiwa ama kutozwa faini
(38%).
Idadi
kubwa ya wananchi pia wanasema kuwa serikali ipate ridhaa ya mahakama
katika kufanya maamuzi yoyote ya kuliadhibu gazeti kwa kutoa taarifa
zenye maudhui yasiofaa (54%).
Japokuwa
wananchi wana mtazamo thabiti kuhusu upatikanaji wa taarifa na uhuru wa
kuzungumza, ni wananchi wachache sana wanaofahamu sheria zinazohusiana
na masuala ya habari. Sheria inayofahamika zaidi katika suala hili ni
Sheria ya Makosa ya Mtandao (2015), ambayo inafahamika na asilimia 10 ya
wananchi huku asilimia 4 pekee ya wananchi wakifahamu Sheria ya Huduma
za Habari (2016).
Wananchi
wengi pia hawajaunganishwa kwenye mifumo ya uraia ambapo ni mwananchi 1
kati ya 4 au pungufu mwenye cheti cha kuzaliwa (25%), kitambulisho cha
uraia (21%), leseni ya udereva (9%) na hati ya kusafiria (5%). Hata
hivyo, karibu wananchi wote (98%) wana vitambulisho vya mpiga kura
Mkurugenzi
Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: “wananchi wanaunga mkono
kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kujieleza. Lakini
ukweli wa mambo ni kwamba, wananchi hawaombi taarifa hizo, wana imani
duni na vyanzo vyote vya taarifa ukiweka kando kauli zinazotolewa na
Rais na Waziri Mkuu, na hawajioni kama wanaweza kuwakosoa viongozi wakuu
wa serikali.”
“Kutokana na kwamba hivi karibuni serikali imepitisha kanuni za Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa
tuna
imani kuwa itakidhi kiu ya wananchi ya kupata taarifa kutoka
serikalini. Tunaishauri serikali kuweka wazi taarifa ili kuyafikia
matarajio ya wananchi. Cha kusikitisha, wananchi wanakamatwa na serikari
kwa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii. Ni vyema serikali ikatambua
thamani ya mijadala huru ya umma na ukosoaji wenye lengo la kujenga
katika mapambano dhidi ya rushwa na katika harakati za kuelekea kuwa
nchi ya uchumi wa kati.”
0 comments:
Chapisha Maoni