RAIS Jakaya Kikwete amesema ukiona Waziri anajisifia kafanya mambo kadhaa kwa uwezo wake, huyo ana matatizo ya ufahamu na ni mpenda sifa, kwa sababu mambo anayoyafanya anatekeleza majukumu aliyopewa na Rais na kwa mujibu wa muongozo aliopewa.
Alisema
hayo jana wakati akiagwa jijini Dar es Salaam na taasisi zilizopo chini
ya Wizara ya Ujenzi, huku akiongeza kuwa vuguvugu za kisiasa
zinazoendelea, ni moto wa mabua ambao hauwaki ukadumu.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye pia
ndiye mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), angekuwa kama
mawaziri hao, angejisifia kwa mafanikio yote yaliyopatikana katika
Wizara alizoziongoza, ikiwemo Wizara hiyo ya Ujenzi.
Katika
hotuba hiyo amesema sifa moja ya Dk Magufuli ni kutambua kuwa akiwa
Waziri, anafanya kazi kwa niaba ya Rais kwa mujibu wa muongozo na
rasilimali alizopewa, ambavyo vimeeleza nini anatakiwa kufanya kama
waziri.
“Sijawahi
kukusikia ukijisifia binafsi maana na wewe ungeweza kabisa kufanya
hivyo kwa sababu barabara zote hizi ungeweza kusema ni mimi nimejenga na
sio Rais… Sasa bila Rais kukuteua na kukupa muongozo na rasilimali
ungepata nafasi ya kujenga hizo barabara?”Alihoji Rais Kikwete.
Alisema
baadhi ya watu wamediriki kusema waliyoyafanya ni wao na sio Rais
aliyewapa muongozo huo kufanya yoliyofanyika na kuongeza:
“Unadhani
Rais atakuja kujenga nyumba? Amekwambia nimekupa hivi hapa na kila mtu
niliyemteua nafanya hivyo na inatangazwa kwenye gazeti la Serikali.”
Rais
Kikwete alisema Rais hana ushindani na Waziri wake na pia Waziri hana
mashindano na Rais kwa sababu Waziri anafanya kazi kwa niaba yake maana
ndiye aliyemteua.
Moto wa mabua
Alisema
CCM imemteua Dk Magufuli kugombea nafasi ya Urais kupitia chama hicho
na ana imani atapita salama kwa sababu ni mtendaji kazi mzuri na kwamba
vurugu zinazoendelea za kisiasa ni moto wa mabua tu
.
“Nina imani chama chetu kimekuteua kuwa mgombea wa urais kwa sababu ni
mtendaji… Taifa litanufaika likipata kiongozi kama wewe, hao wengine ni
moto wa mabua tu hauwaki ukadumu,” alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete alisema ana imani Mungu akijalia Magufuli kuwa Rais basi yale
mambo mazuri aliyoyafanya katika Wizara ya Ujenzi na sekta ulizopata
kuongoza, atatumia maarifa na uzoefu huo kusukuma mbele gurudumu la
taifa mbele.
Alisema
Dk Magufuli kila wizara aliyopelekwa alifanya vizuri, ikiwa ni pamoja
na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Miundombinu na Ardhi ambapo alisaidia
kuondoa ujanja ujanja na kuimarisha nidhamu lakini hakuwahi kusema ni
yeye binafsi ameleta manufaa hayo.
“Kuna
wakati sehemu fulani ina matatizo watu wanasema jamani kwa nini
msimlete Magufuli, tunasema hawezi kuwa kila mahali… Na sekta hii ya
ujenzi ni sekta muhimu na kubwa, nashukuru chini ya uongozi wako
tumeifikisha mahali pazuri,” alisema Rais Kikwete.
Aidha
Rais Kikwete alisema anajivunia kuunganishwa kwa barabara zote za mikoa
na Wilaya nchini katika kipindi cha uongozi wake na hiyo ni kwa
jitihada na usimamizi uliofanywa na Waziri Dk Magufuli.
“Katika
uongozi wangu tumefanikiwa kuunganisha karibu mikoa yote nchini kwa
kiwango cha lami. Jambo hili limewezekana kwa ushirikiano na wafanyakazi
wote pamoja na wataalam wa wizara hii ya ujenzi.”
Kikwete
alisema alipoingia madarakani, bandari ya Dar es Salaam ilikuwa
inasafirisha jumla ya tani milioni 6.7 za mizigo kwa mwaka, lakini hivi
sasa bandari hiyo inasafirisha mizigo zaidi ya tani milioni 15 hadi
mwishoni mwa mwaka huu, bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa
kusafirisha zaidi ya tani milioni 18, kitu ambacho kitaongeza ukuaji wa
uchumi na kuongezeka kwa pato la taifa.
Aidha
alisema kukamilika kwa barabara zote nchini kwa kiwango cha lami
kutawezesha uchumi kukua kwa haraka zaidi na kuifanya nchi kupiga hatua
kubwa ya kimaendeleo kwa siku za usoni.
Rais
Kikwete pia alisema katika kipindi chote cha uongozi wake ameweza
kupambana na changamoto zilizokuwa zikiikabili wizara ya ujenzi na ndio
maana mafanikio haya yamepatikana.
Hata
hivyo, Rais Kikwete alisema mara baada ya kumaliza muda wake na
kukabidhi madaraka kwa rais ajaye, ataondoka na kurejea kijijini kwao
Msoga na kuendesha shughuli za kilimo, ikiwemo kilimo cha mananasi,
mahindi na mazao mengine.
“Nikimaliza
muda wangu wa uongozi na kukabidhi madaraka, nitarudi kijijini na
kwenda kuendesha shughuli za kilimo, na wala sitaki nikiwa kule
mnifuatefuate. Niacheni nikawe mkulima hodari,” alisema Kikwete.
Alisema
sasa taifa linahitaji kiongozi bora zaidi yake ili aweze kuendeleza
pale alipofikia yeye kwani likipata kiongozi dhaifu hata haya mafanikio
yaliyopo yatarudi nyuma.
Kwa
upande wake, Waziri Dk Magufuli alisema katika kipindi chote cha
uongozi wake katika wizara ya ujenzi, ameweza kuyatekeleza vyema
majukumu aliyopewa na rais kwa kushirikiana na wafanyakazi wenzake ndio
maana wamepata mafanikio.
Alisema
japokuwa wizara yake bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini
imeweza kupambana nazo na kufanikisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu
iliyokuwa ikihitajika, Magufuli alisema anatumaini atakapokuwa Rais
atatatua changamoto hizo zaidi kwa sababu anazifahamu vizuri.
Awali
wakiwasilisha mafanikio yaliyofikiwa na taasisi zao zilizopo chini ya
wizara ya ujenzi, watendaji wa taasisi hizo walisema awamu ya nne
imeweza kufanya mambo mengi na ya kuingwa.
Mtendaji
Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema barabara zenye urefu wa
kilomita 5,568 zimejengwa kwa kiwango cha lami katika serikali ya awamu
ya nne na kugharimu Sh trilioni 4.9.
Mfugale
alisema barabara zinazoendelea kujengwa hadi hivi sasa zina urefu wa
kilomita 3,875 ambazo pia zitagharimu Sh trilioni 4 na bilioni 535 na
kwamba jumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 8,600 zimejengwa kwa
kiwango cha lami nchini nzima ambazo ni sawa na asilimia 86 na nyingine
ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Imeandikwa na Regina Kumba na
Emmanuel Ghula.
0 comments:
Chapisha Maoni