Mgombea
wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema endapo
atachaguliwa, atashusha bei ya vifaa vya ujenzi vikiwamo saruji na
mabati kuanzia mwakani akisema tayari kuna viwanda vikubwa ambavyo
vimeshaanza kujengwa nchini.
Akiwahutubia
wananchi wa Namtumbo, Ruvuma jana, Dk Magufuli alisema kuongezeka kwa
viwanda hivyo akitolea mfano wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote ambacho
kitakuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki na kuimarika kwa Barabara ya
Songea – Masasi ambayo makandarasi wapo kazini, kutasaidia kuvutia
wawekezaji na kusisimua biashara katika mikoa ya Kusini.
Akiwa Tunduru, Dk Magufuli aliahidi kuendeleza uchimbaji wa madini ya urani ili yaweze kuchochea maendeleo nchini.
Akiwahutubia
wakazi wa Namtumbo wilayani Tunduru, Dk Magufuli alisema anafahamu
bayana kuwa eneo hilo lina madini hayo hivyo akiingia madarakani,
Serikali yake itaendeleza urani ili kuwasaidia kukuza uchumi wa wananchi
hao.
Katika
mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa CCM mjini hapa, mgombea huyo
alisema iwapo atapatiwa ridhaa hiyo Oktoba 25, ataimarisha uhusiano
mzuri na nchi zote jirani na wafadhili wa maendeleo.
“Tutaendelea
kuuenzi uhusiano mzuri na majirani zetu wanaotuzunguka wa Kenya,
Malawi, Zambia, Msumbiji, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi Sudan Kusini. Pia, kuimarisha uhusiano
na nchi nyingine za Afrika na mabara mengine na wafadhili wetu ambao
wanatuamini sana na kutusaidia,” alisema Dk Magufuli.
Alisema
wafadhili wengi wanachangia katika miradi ya maendeleo ya barabara kwa
sababu wanaiamini Serikali na kuwa fedha hazitaliwa na mafisadi.
Alitokea
mifano ya Barabara za Namtumbo – Tunduru-Mtambaswala zinazojengwa kwa
ushirika na Shirika la Maendeleo la Japan (Jica) na Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), kuwa ni matokeo ya uaminifu katika matumizi ya fedha
za miradi.
“Wafadhili
wanamwamini Magufuli kwa kuwa fedha zikitolewa hazichukuliwi. Hivyo
msilete mtu ambaye haaminiki hata kwa wafadhili, akipatiwa fedha
anakula, halafu akachukiwa na wafadhili baadaye wakasusia kutoa fedha za
kumalizia miradi ya barabara tuliyoianza,” alisema.
Msafara wasimamishwa
Msafara
wa mgombea huyo ulilazimika kusimamia mara nyingi baada ya wananchi
kukaa barabarani kumtaka ajibu kero zinazowakabili, nyingi zikiwa ni za
maji, barabara, umeme na afya.
Tangu
alipoanza safari Songea Mjini, Dk Magufuli alisimama kwenye maeneo
yasiyopungua 12, safari hii akitumia dakika chache tofauti na
alivyofanya katika safari ya Vwawa-Tunduma mkoani Mbeya.
Dk
Magufuli alivuta hisia za wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi wa Barabara
ya Matemanga-Liuli aliposimama katika Kijiji cha Huria wilayani Tunduru
kusikiliza kero zao zikiwamo za mishahara na kumuomba aendeshe mtambo wa
kusawazisha udongo barabarani.
Baada
ya kuujaribu mtambo huo kwa takriban dakika tano, aliwahakikishia kuwa
mkandarasi SRBG atawalipa malipo yao yote kwa kuwa Serikali imeshamlipa
fedha zote za mradi.
Akiwa
Matemanga, aliwaahidi wananchi kujenga kiwanda cha kuongeza thamani za
korosho kwa kuwa utawala wake utakuwa ni wa viwanda.
Huku
akitumia historia ya utendaji wake katika Wizara ya Ujenzi, Dk Magufuli
aliahidi kuwa Barabara ya Namtumbo-Masasi itakamilika mwakani na kuwa
kuna makandarasi wanane wanaoendelea na kazi za ujenzi.
Katika
mkutano wake Mjini Tunduru, Dk Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti
mtarajiwa wa CCM, aliwapokea makada wapya 16 waliodai kuitosa Chadema.
Kutokana
na kusimama mara kwa mara njiani kuzungumza na wananchi, Dk Magufuli
alilazimika kufanya mikutano mifupi zaidi mjini Masasi huku akiwaomba
radhi wakazi wa mji huo kwa kuchelewa.
“Ninafahamu
wananchi wa Masasi mna masikitiko makubwa ya mazao, korosho, stakabadhi
ghalani, ninataka niwaahidi hili nitalighulikia,” aliuambia umati mkubwa wa wananchi katika Uwanja wa Boma na kuongeza:
“Waziri wangu nitakayemteua wa kilimo hili lazima alifanyie kazi.”
Aliwaahidi
wakazi wa mji huo kuwa atajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Masasi
hadi Mtwara kupitia Newala yenye urefu wa kilomita 200.
Alisema
tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo vimeshafanyika na
kilichobaki ni kuanza tu kujengwa kwa kuwa tenda ilishatangazwa.
Alisema kujengwa kwa barabara hiyo na nyinginezo kuiwezesha Tanzania kuwa ya kisasa.
Aliendelea
kutoa ahadi ikiwamo ya mikopo ya Sh50 milioni kwa vikundi vya vijana na
wanawake katika kila kijiji, kujenga reli ya kisasa ya Mtwara-Mbamba
Bay na kuwasomesha bure, watoto kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha
nne.
Kutokana
na ufupi wa muda, Dk Magufuli aliahidi kurejea Masasi endapo
atachaguliwa ili kufanyia kazi masuala mbalimbali yakiwamo ya maji na
mengineyo.
“Ni bahati mbaya ndugu zangu nimefika jioni nisameheni sana nitakuja tena na Mungu awabariki sana,” alimaliza kwa salamu ya Masasi “hoyee”, “Masasi kucheleeee.”
0 comments:
Chapisha Maoni