MAMLAKA
ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya imemtia mbaroni mfanyabishara
wa kemikali bashirifu, mkazi wa Mwanza ambaye alitaka kuwahonga
mamilioni ya fedha makamishna wa mamlaka hiyo ili wavuruge kesi
inayomkabili.
Mfanyabiashara
huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana sababu za usalama,
inasemekana baada ya kukamatwa, aliahidi kumhonga Sh milioni 800
Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rogers Siang’a amsaidie kufuta shitaka
lake.
Pia,
mtuhumiwa huyo aliahidi kumpa rushwa ya Sh milioni 400 Kamishna wa
Sheria wa Mamlaka hiyo, Edwin Kakolaki ili naye amsaidie kuvuruga kesi
iliyokuwa ikimkabili.
Siang’a
alikuwa akizungumza juzi mjini hapa wakati wa semina ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge inayoshughulikia Ukimwi na Dawa za Kulevya.
Alisema
viwango vikubwa vya kemikali bashirifu ambayo mara nyingine hutumika
kutengenezea dawa za kulevya, imekuwa ikiingizwa nchini.
“Kuna
zaidi ya kampuni 2000 zimekuwa zikiingiza kemikali bashirifu nchini
lakini kasi ya kuzikagua kemikali hizo imekuwa ndogo kutokana na wingi
wa kampuni na uchache wa rasilimali watu na fedha.
“Lakini
Desemba mwaka jana, kuna mfanyabiashara mmoja wa kemikali bashirifu
alitaka kumpa hongo Kamishna Kakolaki, ya Sh milioni 400 avuruge kesi,
ila kwangu alisema akinifikia atanipa Sh milioni 800,” alisema
Siang’a.
Kamishna
wa Kinga na Tiba kwenye mamkala hiyo, Dk. Peter Mfisi, alisema hadi
sasa Watanzania 1050 wamekamatwa katika nchi mbalimbali wakituhumiwa
kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Alisema kitendo hicho kimekuwa kikichafua hadhi ya Tanzania katika sura ya mataifa.
“Hata
hivyo, udhibiti wetu umefanikiwa kudhibiti uingizwaji wa dawa hizo
nchini na kusababisha kuongezeka kwa watu wanaohitaji matibabu ya
‘methadone na kupanda kwa bei ya dawa hizo mtaani.
“Kwa
ujumla, hali bado ni mbaya kwa watumiaji wa dawa hizo hasa kutokana na
kuambukizana magonjwa ya Ukimwi, TB na homa ya ini kwa sababu watumiaji
hao wana tabia ya kuchangia sindano.
“Lakini
mtumiaji akimuona mwenzake anasinzia wakati akiwa amejichoma sindano,
basi hunyonya damu ya mwenzake kwa kutumia sindano kisha kujidunga
akiamini kuwa damu ya mtu huyo ina dawa za kulevya,” alisema.
Waziri
wa Nchi, Sera, Uratibu, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama,
alisema kutokana na udhibiti wa dawa hizo kuimarika, wafanyabiashara
wameanza kuwatumia watoto wa viongozi na matajiri wakiamini wana uwezo
wa kununua dawa kwa urahisi.
“Pamoja
na hayo, Serikali itawasaka kila kona bila kujali mtu au nafasi
aliyonayo kuhakikisha mtandao huo unatokomea,” alisema.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Oscar Mukasa, alisema lengo la
semina hiyo ni kuwapa mwanga wajumbe wapya wa kamati hiyo wafahamu
utendaji kazi na muundo wa mamlaka hiyo.
Pamoja na hayo, alisema kamati yake itashirikiana na mamlaka husika na Serikali ili vita dhidi ya dawa za kulevya, ifanikiwe.
0 comments:
Chapisha Maoni