test

Alhamisi, 1 Machi 2018

Kabla Sijafa - Sehemu ya 01 ( Simulizi ya Kweli)



Mwandishi: Grace G. Rweyemam

“Habari Grace. Ninaitwa Ninah, ningependa katika simulizi unazotuma fesibuku, nikupe na wosia wa kaka yangu marehemu, uwaandikie watu. Kabla hajafa aliniomba sana niwambie watu wengi kadiri niwezavyo kile alichotaka wajue. Akaniachia barua ndefu sana aliyoiandika mwenyewe” 
Nilisoma ujumbe huo nikastuka na kutamani kujua huo wosia wa marehemu aliotaka uwafikie watu unahusu nini. Nilimpa anuani yangu ya barua pepe na kumuomba aniandikie huo wosia humo, nijue kama kweli ungefaa kuwafikia watu kama ambavyo marehemu alidai.

Nirudi nyuma kidogo, Kuna mdogo wangu yuko katika kundi moja la fesibuku, la wasichana na wanawake, amekuwa akinisimulia visa kadha wa kadha vinavyowatokea wadada wengi walio kwenye ndoa. 
Mambo mengi ambayo huwa hunisimulia hunifanya nijue kumbe kweli UKIMWI bado upo na unaua. Kuna kisa fulani aliniambia miezi kadhaa iliyopita, kikanifanya nitamani kama watu wengi zaidi wangeelewa uhalisia wa huu ugonjwa na jinsi unavyowamaliza wengi mpaka leo hii, hata wale wasiotegemea. 
Mbaya zaidi kwa sasa ambapo kumekuwa na dawa za kuongeza kinga, wagonjwa wengi wa UKIMWI hawajulikani kwa kuonekana kwa macho, na huo umekuwa mtego kwa watu wengi. 
Kuna binti mmoja, nitampa jina la Vero, kwenye hilo kundi ana ndoa ya miaka mitatu na wana mtoto mmoja, aliwahi kufuma jumbe za mapenzi kwenye simu ya mume wake, mwanaume akawa akijitetea na kuomba msamaha, binti akasamehe.

Siku moja binti aliamua kufuatilia namba, alipofuma tena ujumbe wa mapenzi kwa mume wake, akaja kugundua kumbe ni ya jirani yao, cha kumshangaza zaidi huyo jirani yao ni kijana wa kiume.
 Binti akachanganyikiwa ndipo akaamua kuomba ushauri kwenye hilo kundi, pasipo kujitaja jina lake, watu wakamshauri asamehe, asimfuatilie mwanaume, wengine wakashauri aachane naye, na kuna waliomshauri akapime na akikutwa salama basi amuache. 
Sasa akiwa anafikiria nini cha kufanya, siku mbili baadaye akiwa nyumbani kwake, alitembelewa na jirani yake mwingine nitamuita Siwema. Katika maongezi yule mwanamke Siwema, bila kujua chochote akaanza kuelezea kuwa yule kijana jirani ambaye Vero aligundua kwamba ana mahusiano na mumewe ni shoga na ni muathirika. 
Siwema aliongea kwa malalamiko kuwa kuna mtoto wa dada yake (naye ni wa kiume) alikuja kuishi kwake kwa muda wa miezi mitatu akiwa likizo ndefu ya chuo kikuu, kumbe walianzisha mahusiano na yule mvulana. Sasa anadai siku kadhaa zilizopita amegundulika ameathirika, amechanganyikiwa sana kijana pamoja na mama yake. 
Siwema alisema alishasikia tetesi hapo nyuma kuwa yule kijana ameathirika, ila hakutilia mkazo sana, mpaka alipogundua amemuambukiza huyo mtoto wa dada yake, kwani kijana baada ya kupimwa na kukutwa na UKIMWI alimueleza mama yake ukweli kuhusu ni wapi anahisi ameutoa.

Akielezea tena Vero kupitia kwa kiongozi (admini) wa hilo kundi, alisema, “Nikiwa bado nawaza kuhusiana na ushauri wenu, nilikuja kugundua kuwa yule kijana anayetembea na mume wangu ni kweli ni shoga na ameathirika. 
Nikahamaki sana, nikataka kumwambia mume wangu, ila nikajizuia mpaka nilipoenda kupima, nami nimekutwa nimeathirika. Hapa nimeshalia siku nzima. Mume wangu amesafiri, ila sijui kama nina uvumilivu wa kumngoja mpaka arudi. 
Naumia, natamani hata nimuue yule kijana na mume wangu pia. Namuangalia mwanangu naumia sana. Nimekuwa mwaminifu kwa ndoa yangu na hata sikuwahi kukaa nikawaza ninaweza kufa na UKIMWI”

Watu kama kawaida walimshauri yao, maisha yakaendelea. Sasa kilichokuja kunishangaza ni yule mwanaume alivyojibu baada ya kuambiwa kila kitu na mkewe.
 “Mke wangu, bora hata ungekuwa mkali zaidi kwangu, ungenisaidia kukuheshimu. Ona sasa tunamsababishia mtoto kubaki yatima akiwa mdogo namna hii.” Hiyo sentensi ilinifanya nijiulize kuwa kumbe wakati mwingine kuna mambo huwa si ya kujaribu kuwa muelewa kwa mwenzi wako. 
Nilimfananisha huyu mwanaume na mtoto mdogo, au labda punda, ambaye akiachwa kidogo hujisahau kuwa anawajibika kutembea au kufanya jambo fulani, kitu ambacho si sahihi hata kidogo. Mungu alituumba na utashi, wa kuchagua kufanya mema au mabaya. 
Hakuna mwanadamu ambaye huweza kujitetea kwamba ni kwa sababu sikuhimizwa kutofanya jambo fulani ndio sababu niko hapa nilipo. Maadamu wewe ni mtu mzima, na una akili timamu, basi unawajibika kwa kila unachokifanya kikakusababishia madhara kwenye maisha yako.

Nikitafakari ni namna gani naweza kufikisha ujumbe huu kwa watu, yaani kuhusu UKIMWI, ni kama nilipata bahati tu, au niseme Mungu aliniunganisha na mtu fulani, kupitia hii mitandao ya kijamii, akafanyika njia rahisi ya mimi kuzungumzia hili suala kwa namna ambayo ninaamini nitaeleweka vizuri. 
Mbali na uandishi, kitaaluma mimi ni mwanasayansi ya jamii, yaani nimesomeaa masomo ya afya ya halaiki, hivyo masuala ya afya kama magonjwa yasiyotibika hunihusu kwa ukaribu kabisa. 
Nimekuwa na shauku ya kuwasaidia watu wasiteseke na haya magonjwa, kwani najua kwa undani sana madhara yake. Kwa ambayo hayakwepeki kwa urahisi kama saratani au kisukari, huwezi kumlaumu mtu, ingawa nayo tumejifunza njia mbalimbali za kujikinga.
 Ila kwa ugonjwa kama UKIMWI, hasa kwa wale ambao huhusika kuutafuta, licha ya kampeni zote zimewahi kufanyika kuhusiana na ugonjwa huo, huwa nashindwa sana kuelewa inakuaje watu ni kama hawaelewi.

Nimekutana na watu kadhaa wenye magonjwa hayo yasiyotibika, na msaada mkubwa ambao nimekuwa nikiutoa kwao ni wa kiroho. 
Najua Mungu huponya, ingawa vigezo na masharti lazima vizingatiwe, licha ya kuwa Yeye huponya bure. Katika simulizi fulani ya awali nimezungumzia nguvu za giza nyuma ya magonjwa, na uponyaji wa Mungu, na nisingependa kuzungumzia humu. 
Simulizi hili ni maalumu kwa ajili ya kumkumbusha msomaji kuwa UKIMWI upo na ni muhimu kuchukua tahadhari. 
Nilisoma wosia wa marehemu Bahati machozi yakinitoka. Niliwaza uchungu aliokuwa akisikia akiwa anakata roho, kwani barua yake ilionyesha ni kiasi gani alijutia mno maisha aliyoishi. 
Ila pia nilijifunza mambo kadha wa kadha ya muhimu sana, ambayo ninaamini kila anayepata fursa ya kuusoma wosia huo, atajifunza.

ITAENDELEA KESHO
#TrueStory

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni