Mapokezi
ya mabango yaliyobebwa na wananchi wa eneo la Nyamongo wilayani hapa,
yamesababisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujitwisha mgogoro uliodumu
kwa zaidi ya miaka 15 kati ya wakazi hao na Mgodi wa Dhahabu Acacia
North Mara.
Serikali
imeahidi kutatua mgogoro huo kati ya mgodi na wananchi wanaozunguka
eneo hilo, ili kumaliza uhasama na kurejesha amani kati ya makundi hayo
mawili yanayohasimiana kwa kipindi kirefu.
Ahadi
hiyo ilitolewa jana na Majaliwa alipotembelea eneo la Nyamongo wilayani
Tarime katika ziara yake ya siku saba inayoendelea mkoani Mara.
Hiyo
ni baada ya kupokewa na mabango aliyosema hayapungui 400 alipofika eneo
la Nyamongo, jambo alilosema ni ishara tosha ya kuwapo tatizo
linalowachukiza wananchi linalohitaji ufumbuzi wa Serikali na viongozi
wa ngazi zote.
Kikao
cha kwanza cha kujadili na kutafutia ufumbuzi mgogoro huo
kitakachohusisha wajumbe watano wa watakaowakilisha wananchi, uongozi wa
mgodi, mbunge wa Tarime vijijini (John Heche) na wataalami wa Wizara ya
Madini kitanatarajiwa kufanyika mjini Dodoma Januari 27.
Mambo
muhimu yatakayojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa Waziri Mkuu
ni malipo ya fidia kwa mali ya wananchi, maeneo ya uchimbaji kwa
wachimbaji wadogo, upatikanaji wa mawe (mabaki) ya dhahabu maarufu kama
magwangala.
Mengine
ni upatikanaji wa maji safi na salama eneo la Nyamongo (vyanzo vya maji
vya asili vinadaiwa kuchafuliwa na kemikali), na udhibiti wa matumizi
ya nguvu kupita kiasi, ikiwamo kupiga mabomu ya machozi na risasi
panapotokea mgogoro au vurugu kati ya wananchi na mwekezaji.
“Nimepokewa
na mabango tangu nianze ziara mkoani Mara Januari 15; lakini mabango ya
Nyamongo yametisha. Hayapungui 400 na yote yanaonyesha uhusiano mbaya
kati yenu (wananchi) na mwekezaji. Nitalibeba hili na kulimaliza,”
alisema Majaliwa akiamsha shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi.
Licha
ya amani na utulivu eneo la Nyamongo, uamuzi huo wa Serikali pia
unalenga kuondoa kuviziana kati ya wananchi na vyombo vya dola
vinavyotumika kudhibiti na kurejesha amani na utulivu nyakati za uvamizi
unaofanywa na makundi ya watu, hasa vijana wanaoingia eneo la mgodi
kuchukua mawe au mchanga wa dhahabu.
“Mgogoro
huu unakwamisha juhudi za wananchi, Serikali na wawekezaji katika
kujiletea maendeleo kupitia rasilimali ya madini yanayopatikana
Nyamongo, lazima tuutafutie ufumbuzi wa kudumu kwa faida na masilahi ya
pande zote,” alisema Majaliwa.
Alisema
yeye binafsi ataongoza mazungumzo ya kutatua mgogoro huo hadi mwafaka
utakapopatikana na kuagiza pande zote kuunga mkono juhudi hizo kwa
kufuata sheria, kanuni na taratibu huku maslahi na maendeleo ya wananchi
yakipewa kipaumbele.
Awali,
mbunge wa Tarime vijijini, John Heche alimweleza Majaliwa kuwa uhasama
kati ya wananchi na wawekezaji, kukosekana kwa huduma bora za kijamii
kulinganisha na ya utajiri wa madini eneo hilo na matumizi ya nguvu ya
vyombo vya dola dhidi ya wakazi kwa faida ya mwekezaji bila kujali
uhalali wa madai ya wenyeji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabiliwa
wakazi wa Nyamongo.
0 comments:
Chapisha Maoni