Meya
wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amekanusha uvumi unaomhusisha na
mipango ya kujiondoa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mwita
amesema lengo la uzushi huo ni kumchafua hasa kutokana na staili yake
ya kazi ya kushirikiana na serikali badala ya kupambana katika kutafuta
ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kimeya.
Akisisitiza
historia na utamaduni wa Mkurya ni kukataa kuwa msaliti akasema:
“Naomba ifahamike kuwa hakuna Mkurya ambaye aliwahi kuwa msaliti katika
nafasi yoyote ambayo aliwahi kuwa nayo. Kutokana na historia hiyo,
naomba niaminike na wanachama na wananchi wote kuwa haitakuja kutokea
Mkurya mimi nikakisaliti chama changu.
“Na
kama itakuja kutokea nikafanya hivyo ninaweza kuhatarisha maisha yangu,
familia yangu, na hivyo kujikuta nikiingia kwenye matatizo makubwa
ambayo kimsingi siyo mazuri. Mama yangu ni mjane, kama itafanya hivyo
Chadema wote Mkoa wa Mara hawawezi kuwaacha ndugu zangu salama”.
Meya
huyo amesema hajawahi kudhani wala kufikiria kuhama Chadema na kwenda
kwenye chama chochote cha siasa kwani ametoka nacho mbali tangu mwaka
2004 kwa kukijenga chama hicho kwa gharama zake mwenyewe ambapo
anatambua kuwa chama kimemheshimu kwa kumpa nafasi ya umeya hivyo haoni
sababu ya kuondoka kwani ana nia ya kuwatumikia wananchi.
“Kukaa
kwangu kimya, kutofanya siasa za kiharakati ndani ya Jiji la Dar es
Salaam haimanishi kwamba niko upande wowote ama kukihujumu chama changu.
Ila huu ni mfumo ambao nimeuchagua na kujijengea kwa ajili ya
kuwatumikia wananchi na si kufanya harakati za kisiasa kwa kuwa nina nia
ya kufanya maendeleo ndani ya jiji la Dar es Salaam.
0 comments:
Chapisha Maoni