Waziri
wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla amesema ataendelea kuwepo
ndani ya wizara hiyo kama kilichowafanya watangulizi wake kuondoka ni
masilahi binafsi, kwa kuwa hahongeki, hashawishiki na aliyemteua
analifahamu hilo.
“Sitakuwa
tayari kupoteza heshima yangu, aliyeniteua anajua kuwa mimi ni
muarobaini wa hayo yote, hata nilipoteuliwa walianza kunidhihaki kupitia
mitandao ya kijamii kuwa ninakwenda kuharibikiwa huko, eti kwa sababu
mawaziri hawadumu, haipo hiyo,” alisema Dk Kigwangalla jana Jumapili
Oktoba 22,2017 mjini Dodoma.
Alisema
hayo akijibu kauli ya Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro
aliyemtahadharisha kuwa mawaziri wamekuwa hawadumu ndani ya wizara hiyo
kutokana na kununulika na wadau kwa kuwa kuna ushawishi mwingi.
Hayo
yameibuka kwenye mkutano wa wadau wa sekta mbalimbali zinazofanya kazi
na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao Dk Kigwangalla alikutana nao
akiwa na Naibu Waziri wake, Japhet Hasunga.
Katika
mchango wake, Meya Lazaro alisema, “Niliwahi kumtahadharisha waziri
mwenzako Hamisi Kagasheki kuwa hatadumu katika wizara hiyo kutokana na
wadau kuwa na vishawishi vingi, leo hii naomba kukuambia kuwa sheria
hizo mnazosema kuwa ni mbovu si kweli bali zinakosa usimamizi wa kutosha
kwa sababu ya masilahi ya watu.”
Meya
Lazaro alimtaka waziri kukutana na kila sekta ili kusikiliza kilio chao
akisema ndani ya wizara hiyo kama atapatikana mtu wa kuisimamia vizuri
inaweza kutoa mchango mkubwa ambao haujapata kutokea lakini akaahidi
kuwa watamsaidia ili adumu kuliko mawaziri wengine.
Alisema “Napenda uendelee kubaki katika wizara hii, wewe ni kijana mdogo nisingependa uwe geti la kutokea.”
Mawaziri
waliowahi kuiongoza wizara hiyo ni Anthony Diallo (2005-2006), Profesa
Jumanne Maghembe (2007-2008; 2016-2017), Shamsa Mwangunga (2008-2010),
Ezekiel Maige (2010-2012), Balozi Hamis Kagasheki (2012-2013) na Lazaro
Nyalandu (2014-2015).
Meya
Lazaro alisema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakiitwa na makundi
mbalimbali akitoa mfano wa wawindaji na kuzungumza nao lakini
hushawishika kuegemea huko na wakiitwa na watu wengine huegemea huko,
hivyo kushindwa kubaki katikati ya sekta zote.
Akijibu hoja hiyo, Dk Kigwangalla alisema hana shaka ya aina yoyote kuhusu kupewa wizara hiyo.
Dk
Kigwangalla aliwatahadharisha wadau akisema wanapofika ofisini kwake
wajiandae vyema, vinginevyo anaweza kusimama na kumuacha mtu kama
atagusa suala la rushwa.
“Mimi
sihongeki, kwa hivyo siko tayari kung’oka kwa sababu yoyote ile, kama
ni umasikini ni bora kufa njaa, kwangu fedha haiwezi kunitolea heshima
licha ya kuwa wote tunazitaka,’’ alisema.
Waziri
huyo amejisifu kuwa hata aliyemteua anajua yeye ni muarobaini, hivyo
imani yake ni kubwa kwake na kwa upande wake hatakuwa tayari kuona
akiharibikiwa njiani.
0 comments:
Chapisha Maoni