Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 23 Oktoba, 2017 atawatunuku vyeti wajumbe wa kamati zilizofanya
uchunguzi wa kiwango, aina na thamani ya madini katika makinikia na
baadaye kufanya mazungumzo na kampuni ya Barrick Gold.
Tanzania
na Barrick Gold Corporation zilifikia makubaliano tarehe 19 Oktoba,
2017 na kutiliana saini mkataba wa kutekeleza mwelekeo mpya wa namna
kampuni hiyo itakavyoendesha biashara ya madini ya dhahabu yanayochimbwa
katika migodi yake hapa nchini, pamoja na kulipa Dola za Marekani
Milioni 300 za kuonesha nia njema ya kufidia madai ya upotevu wa mapato
yaliyotokana na biashara hiyo.
Tukio
hili litafanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam kuanzia saa 5:00 asubuhi na
kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio, televisheni na
mitandao mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Oktoba, 2017
0 comments:
Chapisha Maoni