Na: Agness Moshi – MAELEZO.
Ulaji
wa nyama una faida lukuki kwa afya ya binadamu ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa virutubisho vya aina ya protini ambayo ni rahisi kutumika
mwilini, madini mbalimbali (Calcium, Magnesium, Phosphorus, Zinc na
Chuma); vitamini aina ya folic asidi, E, B na B12 ambayo inapatikana
katika nyama pekee.
Nyama
pia inasaidia katika ukuaji na kuongeza afya ya mlaji kutokana na uwezo
mkubwa wa kujenga mwili, kukarabati seli za mwili zilizokufa, kuzalisha
chembe hai mpya, kurekebisha kinga ya mwili, kuongeza damu na
kuimarisha mifupa.
Hata
hivyo faida zote hizo zinapatikana tu, kwa walaji wa nyama iliyo bora
na yenye kiwango. Hivyo ni vizuri wananchi wakazingatia kanuni za ulaji
wa nyama yenye kiwango ili kujiepusha na athari zinazoletwa na nyama
isiyo na kiwango.
Msajili
wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Bi.Suzana Kiango amesema kuwa nyama
yenye kiwango na bora huanzia kwenye utunzwaji wa mifugo wenye
kuzingatia kanuni za uzalishaji bora, unenepeshaji wa mifugo yenye umri
mdogo kwa kuwalisha chakula mchanganyiko kwa muda usiopungua siku 90
kabla ya kuchinja.
Bi.Kiango
amesema kuwa hatua nyingine ni katika uchinjaji ambapo inashauriwa
ufanyike kwenye machinjio bora ambayo yanakidhi viwango vya usafi. Hii
ni pamoja na kuwa na sakafu na kuta zinazosafishika, maji ya kutosha na
sehemu za kuning’iniza wakati wa kuchuna na kupasua.
“Kanuni
za uchinjaji ni pamoja na kupumzisha mifugo ili kuipoteza fahamu na
kumfanya mnyama asiogope na kuzalisha asidi nyingi inayosababisha nyama
kuwa ngumu, pia iwe rahisi kutoa damu yote katika misuli. Uning’inizwaji
wa chune mara baada ya kuchinjwa unasaidia kuondoa damu iliyo mwilini.
Endapo damu haitatoka yote kwenye chune itasababisha nyama kuwa na rangi
nyeusi na kuharibika mapema”, alisema Bi.Kiango.
Madhara
ya ulaji wa nyama isiyo na viwango na bora ni pamoja na kupata magonjwa
ya tumbo, kuharisha na kutapika endapo nyama itapata vimelea vya
magonjwa hayo, kuugua magonjwa ya kuvimba miguu, kifua kikuu, shinikizo
la damu, kisukari na kansa.
Hata
hivyo, Bi. Kiango amesisitiza kuwa magonjwa haya yanaweza kuwatokea pia
watu ambao hawatumii kabisa nyama kwa hivyo si nyama pekee ndio chanzo
cha magonjwa haya japo inaweza kuwa sababu ya mtu kuugua.
“Bodi
imeendelea kutoa elimu kwa watumiaji na wachinjaji wa nyama kupitia
vyombo mbalimbali vya habari kama vile, redio, televisheni na magazeti.
Pia katika maonesho mbalimbali kama Saba saba na Nane nane ambapo
wataalamu wa bodi hutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea mabanda ikiwa
ni pamoja na kusambaza vipeperushi” amesema Bi.Kiango.
Namna
nyingine ya kutoa elimu ni pamoja na kutumia matamasha ya nyama choma,
wiki ya mayai na maonesho ya kuku, wiki ya chakula salama na siku ya
chakula duniani. Wakati wa shughuli hizi wanashiriki hupatiwa elimu
kuhusu faida na athari za kula nyama isiyo na viwango ili kunusuru afya
zao.
Aidha
walaji huelekezwa maeneo mbalimbali wanayoweza kupata nyama hiyo, na
kwa upande wa wafanyabiashara wa nyama hupewa maelekezo ya kuboresha
miundombinu ya kuzalisha, kuchinja na kuuza kwa kuzingatia viwango vya
ubora na usalama.
Kutokana
na baadhi ya wafanyabiashara ya nyama kuendelea kuwauzia walaji nyama
isiyo na viwango kwa kujua au kutojua madhara ya nyama hizo, Bi.Kiango
alisema kuwa Bodi inachukua hatua za kuhakikisha wafanyabiashara hao
wanapata uelewa wa kutosha.
“Bodi
imeanza kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
ambao watashiriki katika kutekeleza majukumu ya Bodi ikiwa ni pamoja na
kusimamia uzalishaji wa nyama na kuelimisha wachinjaji ,walaji na wadau
wengine wanaojishughulisha na uzalishaji wa nyama”alifafanua Bi.Kiango.
Aliendelea
kusema mafunzo hayo yameshatolewa kwa vitendo kwa watumishi wanne
kutoka katika kila Mamlaka za Serikali za Mitaa za mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma ambapo hadi sasa jumla ya wadau 490
katika maeneo tajwa wamekwisha patiwa elimu hiyo. Pia mafunzo yanatolewa
na wadau wengine ambao ni Chuo cha nyama cha VETA, Dodoma na Kampuni ya
nyama ya jijini Arusha.
0 comments:
Chapisha Maoni