Jeshi
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limetoa tahadhari kwa watumiaji
wote wa barabara nchini kuzingatia sheria ili kuepuka ajali hususani
wakati wa sikukuu ya Eid el Fitri.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana juni 25, 2017, Kaimu
Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani, (SACP) Fortunatus Musilimu
alisema kuwa katika kipindi cha sikukuu madereva wamekuwa wakiendesha
magari kwa mwendo kasi, kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari
na kubeba abiria kupita kiasi hali inayoweza kusababisha ajali.
“Tutafanya
operesheni kali barabarani, kuwapima madereva kiwango cha ulevi na
watakaobainika wamelewa watakamatwa na kuwekwa mahabusu na kufikishwa
mahakamani, nasisitiza kwamba,dereva anayetaka kuendesha gari asinywe
pombe,akitaka kunywa pombe asiendeshe gari” alisisitiza Kamishna
Musilimu katika taarifa hiyo.
Wamiliki
wa magari wametahadharishwa yatakayokodishwa kwenda maeneo ya Fukwe
bila kibali yatakamatwa na wahusika kufikishwa mahakamani.
Kamishna
Musilimu pia alitoa wito kwa wazazi kuangalia usalama wa watoto wao na
wasiwaache wakatembea peke yao barabarani bila uangalizi ili kuepuka
ajali zinazoweza kuepukika.
Akizungumzia
upande wa madereva wa Pikipiki (Bodaboda) alieleza kuwa wamekuwa
wakipita taa nyekundu, wakiendesha pikipiki zao bila kuvaa kofia ngumu,
kubeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) na abiria hao kutovaa kofia
ngumu hivyo kuhatarisha Usalama wao hivyo hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
Kamishna
Musilimu alisema, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani
limekuwa likihamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa
kuzingatia sheria na matumizi sahihi ya barabara ili kuepuka ajali
katika kipindi chote na hasa wakati huu wa sikukuu.
0 comments:
Chapisha Maoni