Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January
Makamba amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuwadhibiti
maofisa watendaji wa vijijiji na kata ambao wamekuwa wakitafsiri tofauti
maagizo ya viongozi na kufanya maamuzi yanayowaumiza wananchi.
Akizungumza
kwenye kikao cha siku moja kilichowakutanisha wabunge wa mkoa wa
Iringa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa na wilaya zote
pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa na madiwani, alisema maamuzi yao
yamekuwa yakiwalazimu wananchi kuichukia Serikali na CCM.
Kikao
hicho kilikuwa maalumu kwa ajili ya kutoa msimamo na mapendekezo ya
Serikali kuhusu kilimo cha umwagiliaji kinachofanywa kwenye maeneo
yaliyokaribu na vyanzo vya maji lengo likiwa kuokoa uharibifu wa vyanzo
hivyo.
“Ninaomba
mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote mpo hapa,
muwadhibiti watendaji wa vijiji na kata ambao wanakuwa na tafsiri zao
binafsi kuhusu maelezo ya viongozi, wakati mwingine wanatuharibia sisi
Serikali au sisi tunaovaa jezi za kijani wana CCM,” alisema Makamba.
“Wamekuwa
wakiweka mambo yao na kuongeza vitu vyao, ukali wao ambao hauna sababu
yoyote na wakati mwingine kutunga faini ambazo hazipo katika utaratibu
na pia huwa na mahakama zao wanakuwa wao ndio waendesha mashitaka na
mahakimu, nawasihi muwaite watendaji na muwaeleza na yule atakayeendesha
jambo hilo kinyume na utaratibu achukuliwe hatua,”alisema.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masena alisema hakuna
mtendaji atakayepona endapo atagundulika kutekeleza shughuli za serikali
kinyume na utaratibu.
Akizungumza
kwa niaba ya wabunge wenzake Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto
aliipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kuwataka wale waliokwishalima
maeneo yaliyokaribu na vyanzo vya maji kuendelea na shughuli zao hadi
hapo Serikali itakapokamilisha mchakato wa kutambua na kubaini maeneo
yanayostahili kuachwa.
0 comments:
Chapisha Maoni