test

Alhamisi, 29 Juni 2017

Watanzania 500 Watimuliwa Kenya


Uhusiano  kati ya Tanzania na Kenya umeanza kuingia dosari baada ya uongozi wa Kaunti ya Kajiado kuwamuru Watanzania zaidi ya 500 wanaoishi kwenye mpaka wa Namanga  kuondoka katika eneo hilo.

Hatua hiyo ya Kaunti ya Kajado  kuwafukuza Watanzania hao imetokana na Serikali ya Tanzania kupitia Idara ya Uhamiaji kudhibiti raia wa Kenya waliokuwa wakiingia nchini holela kupitia mpaka wa Namanga wilayani Longido Mkoa wa Arusha.

Uamuzi huo wa Kenya unatajwa kuathiri uhusiano wa  jamii za   pande mbili za nchi hizo uliojengewa kwa zaidi ya miaka 60 ambako wananchi wamekuwa wakipita kwenda kila upande  kununua bidhaa bila kuzuiwa.

Baadhi ya Watanzania waliofukuzwa   Kenya  walisema  uamuzi huo wa Kaunti ya Kajiado, umewasababishia hasara kutokana na uwekezaji waliofanya nchini humo.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo, alisema akiwa kiongozi na mwakilishi wa Rais Dk. John Magufuli anatekeleza sheria za nchi.

Aliwataka wananchi wanaotaka kuishi nchi yoyote   wafuate sheria za nchi husika na si vinginevyo.

“Ikiwa wazazi wanataka watoto wao wasome   Kenya wafuate sheria za Kenya na Wakenya wakitaka kuingia Tanzania wafuate sheria za Tanzania. Huu ndiyo utaratibu na si vinginevyo,” alisema DC Chongolo.

Raia wa Kenya wanasema hatua ya kufukuzwa kwa Watanzania nchini humo imetokana na Serikali ya Tanzania  kuwafukuza wananchi wa nchi hiyo Machi mwaka huu.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni