Risasi
tano zimetumika kuwaua Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangwi na Ofisa
Mtendaji wa kijiji hicho, kisha kumjeruhi machoni Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Londo, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.
Waliofariki
katika tukio hilo ni Ofisa Mtendaji, Mwarami Shamte aliyekutwa na
majereha matatu ya risasi na Mwenyekiti wa Kijiji, Hamis Bakari Mkima
aliyekutwa na jeraha moja.
Pia wauaji hao walimpiga, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo, Michael Martin risasi ya macho, iliyoharibu macho yake mawili.
Kama hiyo haikutosha, waliichoma moto nyumba ya Martin na kisha kutokomea kusikojulikana.
Mganga wa zamu katika Kituo cha Afya Kibiti, Dk Sadock Bandiko alithibitisha kuuwawa kwa viongozi hao wa kijiji hicho.
Amesema Shamte amekutwa na majeraha matatu yaliyotokana na kupigwa risasi.
“Shamte alipigwa risasi moja kichwani na risasi mbili tumboni,”amesema.
Kwa
upande wa mwenyekiti wa kijiji hicho, Dk Sadock amesema marehemu
alipigwa risasi moja ya shingoni aliyopigwa toka upande wa kulia na
kwenda kushoto lakini haikutokeza.
Pia
alisema mwenyekiti huyo alikuwa na jeraha kubwa katika mguu wake wa
kushoto lililotokana na kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Mganga
Mkuu wa Hospital ya Mchukwi, Dk Zacharia Lukeba alipolazwa Martin,
amesema alipigwa risasi moja ya kichwani iliyofumua na kuharibu kabisa
macho yake.
Amesema tayari wamempa rufaa kwenda Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Mmoja
wa ndugu za marehemu hao amesema watu wanne waliokuwa na bunduki wakiwa
wamevaa nguo nyekundu na kuficha sura zao kwa soksi walivamia kijijini
hapo saa nne usiku wa kuamkia jana.
Amesema
watu hao walianza kwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho (Hamis Bakari
Mkima) (30) ambaye alifanikiwa kuwakimbia kabla hawajamfikia.
Amesema
watu hao walimpiga na kitu chenye ncha kali katika mguu wake wa kushoto
kisha kumrejesha kwake huku wakimtaka awapeleke kwa viongozi mbalimbali
wa kijiji hicho.
Alieleza
kuwa baada ya hapo walimtaka awapeleke kwa Ofisa Mtendaji wa kijiji
hicho (Mwarami Shamte) (40) na baada ya kufika huko walimpiga risasi
tatu na alifariki dunia papo hapo.
Amesema
watu hao bado walimtaka mwenyekiti huyo awapeleke kwa Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Londo na baada ya kufika kwake walimpiga risasi ya usoni
iliyoharibu macho yake.
Amesema baada ya hapo walimpiga risasi moja mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Mangwi, (Hamis Mkima) na alifariki papo hapo.
Pia
ameeleza kuwa wakati watu hao wakifanya hayo walikuwa tayari wamechoma
moto nyumba ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo kwa kutumia mafuta ya
petroli yaliyokuwemo kwenye pikipiki yake na kuteketeza kabisa nyumba
yake yote.
Mdogo
wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo (aliyepofuliwa macho)
aliyejitambulisha kwa jina la Paul Martin amesema tukio hilo limetokea
usiku wa jana saa 4 ikiwa ni muda mfupi tangu aagane na kaka yake.
“Nilikuwa
nyumbani kwake na nimeondoka wakati huo huo kwenda kulala baada ya
dakika chache kupita, tulianza kusikia kelele za watu nisiowafahamu
wakiwa kwenye nyumba ya kaka yangu,” amesema.
Paul
amesema baada ya kusikia kelele hizo alitoka nje ili ashuhudie lakini
kabla hajafanya lolote aliwekwa chini ya ulinzi kwa kumulikwa tochi na
kutishiwa kupigwa risasi.
"Niliona watu kama watano wakiwa na silaha ambao waliniweka chini ya ulinzi baada ya kunimulika tochi," alisema.
Amesema baadhi ya watu hao walikuwa ndani ya nyumba ya kaka yake wakiendelea kumhoji huku wakiwa wamefunika sura zao.
Ameongeza kuwa baada ya hapo watu hao waliondoka na kaka yake kwenda kusikojulikana na baada ya muda mfupi walirudi naye.
Amesema
watu hao baada ya kurejea naye waliwaamrisha watoto wake waliokuwa
wamelala kutolewa nje kisha walichukua mafuta ya petroli yaliyokuwa
kwenye pikipiki ya kaka yake kisha kuyamwaga ovyo kwenye nyumba hiyo na
kuichoma moto.
Amesema
baada ya tukio hilo waliondoka naye kwa mara ya pili na kwenda naye
kusikojulikana kisha wakampiga risasi ambayo imeharibu macho yake yote.
Amesema
baada ya kumpiga risasi hiyo walimtelekeza katika barabara iendayo
katika kijiji cha Misimbo ambapo walimkuta jana asubuhi akiwa
hajitambui.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea kwa matukio hayo.
0 comments:
Chapisha Maoni