Na Dotto Mwaibale
CHAMA
cha Wananchi (CUF), kinatarajia kumfikisha mahakamani Wakala wa
Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kukiuka taratibu za sheria ya
wadhamini kwa kutojiridhisha juu ya uhalali wa majina ya Bodi ya
Wadhamini yaliyofikishwa kwake kama yalipitishwa na kikao halali cha
chama kwa mujibu wa katiba.
Kauli hiyo ameitoa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seifjijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema
wanachukua hautua hiyo kutokana RITA kushindwa kutumia mwongozo na
weledi katika kutekeleza majukumu yao na badala yake wamesukumwa na
utashi binafsi kwa ajili ya hujuma dhidi ya chama hicho.
“Chama
chetu kimepatwa na mshituko mkubwa sana, kuona taasisi kubwa na nyeti
yenye dhamana kubwa katika nchi inaweza kufanya vitendo vya ovyo. RITA
ni taasisi inayobeba maisha ya watu ya kila siku. Licha ya kusajili Bodi
za Wadhamini, inasajili vizazi na vifo, ndoa, talaka na inatunza wosia
kwa ajili ya mirathi,” alisema Maalim.
Alisema michakato wa kufungua kesi hiyo inaanza leo ambapo alieleza kuwa tayari wamekwisha agiza mwawakili kulishughulikia.
Kutokana
na matarajio ya ufunguzi wa kesi hiyo watawasilisha maombi mbele ya
Mahakama Kuu kuitaka isimamishe kesi nyingine zote walizofungua
kuhusiana na kadhia hiyo hadi hapo shauri linalohusu uhalali wa maamuzi
ya RITA litakapoamuliwa.
Maalim
alisema kusajiliwa kwa bodi hiyo ambayo aliiita kuwa ni bodi feki,
alieleza kwamba ni mwendelezo wa kukihujumu na kukidhoofisha chama
kunakofanywa dola kupitia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na
Profesa Ibrahim Lipumba na kundi lake.
Alitaja
mambo manne ambayo yalikuwa msukumo wa kusajiliwa kwa bodi hiyo.
Alisema kuwa ni kwa ajili ya kufuta kesi zote zilizofunguliwa na ambazo
zinawaelemea licha ya kutumia nguvu kubwa ya dola, kufungua akaunti mpya
ya benki ili kumwezesha Profesa Lipumba kupata ruzuku.
Aliongeza
mengine kuwa ni Bodi hiyo kuwezesha udhibiti wa Ofisi za Makao Makuu,
Zanzibar pamoja na kumwondoa madarakani Katibu Mkuu Maalim Seif Hamad na
hivyo kufanikisha njama za kuwapokonya haki Wazanzibar kwa maamuzi yao
ya Oktoba 25 mwaka 2015.
Hamadi alisema kamwe haki ya Wazanzibar haitapotea na kuahidi kuwa ndani ya miezi mitatu haki hiyo itakuwa imepatikana.
0 comments:
Chapisha Maoni