Viongozi
wa dini wametangaza maombi ya siku saba nchi nzima kumwombea Rais John
Pombe Magufuli ili aendelee na juhudi zake za kulinda raslimali za
watanzania kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Hayo
yalisemwa jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu
kwa jamii ya dini zote, Askofu William Mwamalanga kwa niaba ya viongozi
wa dini.
“Tumeamua
kufanya maombi ya siku saba kwa kumtaka kila mtanzania popote alipo
kutembea hatua saba kila siku akimwombea Mhe. Rais Magufuli ili Mungu
amlinde pamoja na anaofanyanao kazi kwa usahihi (uaminifu)”, alisema Askofu Mwamalanga.
Ndani ya siku hizo saba kila mtanzania atakuwa ametembea jumla ya hatua 49 akimwombea Rais Magufuli na wazalendo wenzake.
Kwa
mujibu wa Kiongozi huyo wa Dini, maombi hayo yataanza leo Alhamisi Juni
15 nchi nzima na yatajumuisha watu wa dini zote nchini, yaani madhehebu
ya Kiislam, Kikristo, Kihindu, Budha na madhehebu mengine.
Maombi
haya yanafanyika baada ya kuona kuwa Mhe. Rais Magufuli anachukua hatua
madhubuti za kutaka waliohusika kwa namna yoyote kuiba raslimali za
Taifa hususani madini, wanachukuliwa hatua na kuitaka kampuni ya ACCASIA
kulipa kile ambacho walichukua kinyume cha sheria.
Askofu
Mwamalanga alisema kuwa Kamati yake inamwomba Rais Magufuli achukue
hatua za haraka kudhibiti raslimali za nchi kwa upande wa Wizara ya
Maliasili na Utalii ambako mali nyingi zinatoroshwa na wajanja wachache.
Kamati
hiyo ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini
zote imemwomba Mhe. Rais aziunganishe Wizara za Nishati na Madini na
Maliasili na Utalii na kuunda wizara moja ambayo itasimamia kwa karibu
raslimali za watanzania.
“Tunamwomba
Rais Magufuli amchague mtu makini na mzalendo mwenye uchungu na nchi
hii ili asimamie wizara hiyo, na nina hakika wizara hiyo ikisimamiwa
vizuri, ndoto ya Rais ya kuifanya Tanzania kuwa nchi mhisani itatimia
kwa kuwa hapa Mungu ametujalia kila kitu”,alisema Askofu Mwamalanga.
Viongozi
hao wamempongeza Rais Magufuli kwa Uzalendo na Ujasri alionao katika
kulinda raslimali za Taifa na kupambana na maovu. Wamesema ni kiongozi
wa kuigwa na Marais au viongozi Duniani kote.
Kuhusu
suala la walioachishwa kazi kutokana na kuwa na vyeti feki, Askofu
Mwamalanga alisema kuwa Kamati inamwomba Mhe Rais kuwasamehe wale ambao
wameitumikia nchi hii kati ya miaka mitano na 30 ili walau wapatiwe
kifuta jasho licha ya kwamba walitumika bila kuwa na vyeti halali vya
Kidato cha nne.
“Msamaha
tunaoomba si wa kuwarudisha kazini bali tunaomba kwa ajili ya kupata
kiinua mgongo kwani wengine walitumika kwa uaminifu na hata kupewa tuzo
za ufanyakazi hodari (bora) hasa katika sekta za Afya,wauguzi, Elimu na
maeneo mengine”, alisema Askofu Mwamalanga.
Mapema
wiki hii, Rais Magufuli alipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa
makinikia ambayo iliwajumuisha wanasheria na wachumi. Katika ripoti hiyo
ilibainika kuwa kiasi kikubwa cha madini kilichukuliwa bila watanzania
kupata chochote. Takriban madini yenye thamani ya shilingi trilioni 108
yalisafirishwa nje ya nchi bila Tanzania kupata faida kutokana na madini
hayo.
0 comments:
Chapisha Maoni