Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan
amewaagiza wapelelezi na waendesha mashtaka nchini waepukane na vitendo
vya rushwa bali wafanye kazi kwa bidii kwa kuweka maslahi ya Taifa mbele
kwa kuchukua hatua stahiki kwa watu wanaoiba rasilimali za Taifa.
Makamu
wa Rais ametoa kauli hiyo wakati anazindua mwongozo kwa wapelelezi na
waendesha mashtaka wa kesi za wanyamapori na misitu katika ukumbi wa
Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.
Makamu
wa Rais amesema mwongozo aliouzindua utasaidia kwa kiwango kikubwa
uboreshwaji wa upelelezi na uendeshaji wa kesi zinazohusu wanyapori na
misitu nchini.
“Uwepo
wa mwongozo huu ni dhahiri unategemewa kutoa matokeo chanya katika
mapambano dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu yetu,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Makamu
wa Rais amesema kuwa ana imani mwongozo huo aliouzindua utasaidia
kukomesha vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikiisababishia Serikali
hasara kubwa ikiwemo uharibifu wa rasilimali za Taifa na kupoteza mapato
ambayo yangesaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini.
Kuhusu
sekta ya utalii nchini, Makamu wa Rais amesema pamoja na sekta hiyo
kuliingizia Taifa mapato mazuri lakini inasikitisha kuona kuwa uwepo wa
wanyamapori ambao ndio nguzo kuu ya sekta ya utalii unazidi kupungua
kila kukicha hivyo kuwa tishio kubwa kwa uchumi na nchi.
Amesema
vitendo vya ujangili vimeendelea kuangamiza wanyama hasa tembo, hivyo
ni muhimu kwa wapelelezi na waendesha mashtaka kutenda haki bila kuonea
mtu kwa watu wanaokamatwa kufanya vitendo hivyo ili viweze kukomeshwa
nchini.
“Wazee wetu walilinda na kutunza rasilimali zetu kwa faida yetu nasi tuzitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo,” ameeleza.
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa kazi ya kupambana na ujangili na
utoroshaji wa wanyama na viumbe wengine itakuwa endelevu na wale wote
watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha
vitendo hivyo.
Waziri
Profesa Maghembe amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini kuendesha
operesheni maalum ya kukusanya silaha zote ambazo zimekuwa zikitumika
kwenye ujangili ili kuhakikisha wanyama hasa tembo wanakuwa salama
kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa nchini.
Naye,
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amefafanua kuwa
katika kipindi cha mwaka 2014-2017 ofisi yake imewafikisha Mahakamani
washtakiwa wakubwa wa ujangili ambao walihukumiwa vifungo virefu na
faini.
Amesema
kuwa washtakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya zaidi ya shilingi
bilioni 1.1 kwa kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria na
faini hizo zimeshalipwa Serikalini.
Ameeleza
kuwa kati ya idadi hiyo watuhumiwa zaidi ya 80 walihukumiwa kifungo cha
miaka 20 hadi 30 gerezani na faini ya zaidi ya shilingi milioni 164
ambazo bado hazijalipwa Serikalini.
Mwendesha
Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amesema mafanikio hayo yote
yamechangiwa na usimamizi madhubuti wa kesi hizo kupitia dawati la
wanyamapori katika Divisheni ya Mashtaka pamoja na Mawakili wa Serikali
katika Ofisi zote za mikoani nchini.
Ameeleza
kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye kazi kwa sasa ni dhamana
kwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo vya ujangili ambapo utafiti
uliofanywa Mahakama za mkoa wa Dar es salaam tu katika kipindi cha mwaka
2010 hadi 2015 unaonyesha kuwapo kwa jumla ya mashauri 13
yanayohusishwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi
milioni 800 zilizokamatwa ndani na nje ya nchi ambapo watuhumiwa wake
walipewa dhamana na kutoweka.
Biswalo Mganga amesema katika mashauri hayo, asilimia 69 walikuwa ni raia wa kigeni na asilimia 31 ni raia wa Tanzania.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ikulu – Dar es Salaam.
0 comments:
Chapisha Maoni