Tarehe
24 Aprili, 2017 magazeti nchini Kenya yalitoa taarifa ya kwamba
Serikali ya Kenya itapiga marufuku uingizwaji wa gesi ya kupikia
(Liquefied Petrolium Gas, LPG) nchini humo kutokea Tanzania, na kwamba
gesi itakayoruhusiwa kuingia Kenya ni ile itakayokuwa imepitia kwenye
Bandari ya Mombasa peke yake.
Baada
ya kusoma taarifa hizi Serikali ya Tanzania iliwasiliana na Serikali ya
Kenya ili kupata maelezo kuhusu hatua hii ambayo ni kinyume cha
taratibu za kibiashara katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Tarehe 18 Mei, 2017 Serikali ya Kenya ilitekeleza uamuzi wake kwa kuzuia shehena ya gesi isiingie Kenya kutokea Tanzania.
Hatua
hii ina athari kubwa kwa wafanyabiashara wa gesi ya kupikia hapa nchini
pamoja na watu wote ambao ajira zao zinategemea biashara hii.
Wakati hatua hizi zinachukuliwa bado Serikali ya Kenya ilikuwa haijatoa maelezo rasmi kwa Tanzania kuhusu uamuzi wake huo.
Katika
kikao cha Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na
Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kilichofanyika tarehe 2
Juni, 2017, suala la hatua ya Kenya kupiga marufuku uingizwaji wa gesi
kutokea Tanzania lilizungumzwa kwa kirefu na kufanyiwa maamuzi.
Kimsingi
Serikali ya Kenya ilikubali kuondoa katazo la uingizaji wa gesi kupitia
Tanzania mara moja, na makubaliano haya yaliingizwa kwenye kumbukumbu
za Mkutano ambazo ziliafikiwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya kwa
kuweka sahihi.
Pamoja
na makubaliano haya, Kenya imeendelea kuzuia gesi isiingie nchini mwao
kutokea Tanzania. Serikali ya Tanzania imewasilisha rasmi malalamiko
yake Kenya kuhusu suala hili.
0 comments:
Chapisha Maoni