Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa
Sheria ya Bunge, Sura 129, ili kusimamia na kuratibu utoaji wa mafunzo
ya elimu ya ufundi nchini.
Jukumu
kubwa la Baraza ni kuendeleza na kuinua ubora wa elimu na mafunzo ya
ufundi nchini kwa kusimamia kikamilifu shughuli za usajili na ithibati,
mitaala na upimaji ili tuzo zitolewazo na vyuo/taasisi ziwe na ubora
unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Kifungu
cha 5 (1) (e) na (f) cha Sheria hii kinaipa mamlaka NACTE, kuanzisha
tuzo mbalimbali zinazotolewa na kuhakikisha kuwa ubora wa elimu na
mafunzo ya kada ya kati yatolewayo na taasisi mbalimbali yanazingatia
ubora unaokusudiwa.
Aidha,
Kifungu cha 11, kinalitaka Baraza kuhakikisha kuwa Tuzo zitolewazo na
vyuo na taasisi zote zinazoendesha mafunzo ya kada ya kati zinatambuliwa
na mamlaka husika. Katika muktadha huu, kila chuo/taasisi inayotoa
elimu ya ufundi inatakiwa kuwasilisha Baraza matokeo ya mitihani kila
mwisho wa semista.
Hivyo,
kwa kuwa Udahili na uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya
Shahada mbalimbali yanayotolewa na taasisi/vyuo vyote hapa nchini,
utafanyika moja kwa moja vyuoni, Baraza linao wajibu wa kuziwezesha
taasisi/vyuo hivyo kudahili wanafunzi wenye sifa stahiki.
Ili
kulifanikisha hili, Baraza limeandaa mfumo ambao taasisi/chuo kitapata
taarifa za muombaji mwenye sifa linganifu (muhitimu wa Stashahada) moja
kwa moja.
Hivyo,
wahitimu wote wa Stashahada yoyote wanaokusudia kuomba kujiendeleza
katika ngazi ya Shahada wanatakiwa kuhakiki taarifa zao Baraza (NACTE)
kabla ya kufanya maombi yao kwenye taasisi/vyuo wanavyotaka kwenda
kusoma.
Uhakiki
huo utafanywa kwa njia ya mtandao (online) kupitia Mfumo wa Uhakiki wa
Tuzo (NACTE Award Verification System - NAVS) kwa kubofya hapa au kupiti
tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz) kwa kubofya kitufe kilicho andikwa Award Verification.
Baada
ya kuhakiki taarifa zake kuwa kamilifu na sahihi, mhakiki atapatiwa
Namba ya Utambulisho (Award Verification Number - AVN) ambayo
itaambatanishwa na maombi ya Udahili kwenye taasisi/chuo husika.
Utambulisho
huo utatumiwa na taasisi/chuo kujiridhisha kwamba taarifa
alizowasilisha muombaji wa Udahili ni sahihi na hivyo kuweza kudahiliwa
na kisha kuchaguliwa kwa ajili ya masomo kulingana na mahitaji ya
taasisi/chuo husika.
Aidha,
Baraza linapenda pia kuwafahamisha wale wote walio na Stashahada
walizopata nje ya nchi (Foreign Diploma Awards), nao waziwasilishe
kupitia mfumo huu (NAVS) kwa ajili ya kuzifanyia ulinganifu na kuweka
taarifa zao kwenye Kanzidata ya Baraza ili nao waweze kupata Namba ya
Utambulisho. Maelezo ya namna ya kuziwasilisha tuzo za kufanyiwa
ulinganifu yanapatika kwenye tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz).
Ili
mwombaji Udahili apate Namba ya Utambulisho atalipa Shilingi Elfu Kumi
(10,000/=) kwa njia ya mtandao (Online) kwa kufuata maelekezo yaliyopo
kwenye Mfumo wa Uhakiki wa Tuzo - NAVS.
Kwa
wale wanaotaka kufanya ulinganifu wa vyeti vyao, watatakiwa kulipa
Shilingi Elfu Ishirini (20,000/=) kwa tuzo za ndani ambazo hazisimamiwi
na baraza, na Shilingi Elfu Hamsini (50,000/=) kwa tuzo za nje ya nchi
(foreign awards).
Baraza
linapenda kuwafahamisha wahitimu wa Stashahada wanaotaka kujiendeleza
katika ngazi ya Shahada kuwa wanaweza kufanya uhakiki huo kuanzia leo
tarehe 28 Juni, 2017 hadi tarehe 20 Julai, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)
TAREHE: 28/06/2017
0 comments:
Chapisha Maoni