Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ametuma salamu za rambirambi kwa familia, wanachama wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), uongozi wa Klabu ya Yanga na wanamichezo wote kwa
ujumla kufuatia kifo cha shabiki mkubwa wa timu ya Yanga Bw. Ali Mohamed
maarufu kwa jina la Ali Yanga.
Ali
Yanga amefariki dunia jana tarehe 20 Juni, 2017 kwa ajali ya gari
iliyotokea katika Kijiji cha Chipogolo kilichopo katika Wilaya ya
Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Mhe.
Rais Magufuli atamkumbuka Ali Yanga kwa uzalendo wake na mchango wake
wa kuhamasisha na kushabikia masuala mbalimbali ya kitaifa na hasa
michezo, ikiwemo kuishabikia timu yake ya Yanga, timu ya soka ya Taifa,
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na shughuli za kiserikali kama vile Mwenge wa
Uhuru na ziara za viongozi.
“Nimeguswa
sana na kifo cha Ali Yanga, nilikuwa nae wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 ambapo alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa
wananchi kukipigia kura chama changu cha CCM, na pia amekuwa akiongoza
mashabiki wenzake kuishabikia timu ya Yanga na timu ya Taifa bila
kuchoka. Kwa kweli alikuwa hodari sana katika ushabiki wake.
“Natoa
pole nyingi sana kwa familia yake, viongozi wa timu ya Yanga,
wanamichezo wote, wana CCM na wote walioguswa na kifo cha Ali Yanga na
namuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi,
Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kibaha, Pwani.
21 Juni, 2017
0 comments:
Chapisha Maoni